• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 6:50 AM
Ufanisi dhidi ya pombe haramu Mlima Kenya ilikuwa hekaya tu?

Ufanisi dhidi ya pombe haramu Mlima Kenya ilikuwa hekaya tu?

NA MWANGI MUIRURI

HUKU Naibu wa Rais Rigathi Gachagua akipigia upatu vita dhidi ya ulevi kiholela na mihadarati Mlima Kenya alivyozindua mapema 2023 akidai vimezaa matunda, hali katika Kaunti ya Murang’a inamkosoa.

Kwa mfano, Bw Gachagua alikuwa amependekeza baa zipunguzwe katika kaunti hiyo, wale wanaokiuka sheria za vileo wakamatwe, waandalizi na wachuuzi wa pombe haramu watiwe mbaroni na wanaouza mihadarati waadhibiwe kisheria.

Licha ya Naibu wa Rais kudai kwamba kero ya ulevi imedhibitiwa na vijana wameanza kuoa na kuzaa, hakuna utafiti rasmi umefanyika kuthibitisha kauli yake, huku vijana wengi wakizidi kuonekana mitaani wakiwa walevi chakari.

“Lakini ulevi kiholela umezidi kuwa kero kuu na kuteka vijana wetu wa jinsia zote, familia zinazidi kulia wamiliki wa baa wakiendeleza njama zao za kujiweka juu ya sheria kupitia hongo,” anateta Mwenyekiti wa Wazee wa Agikuyu eneo la Murang’a Mwangi Kiragu.

Kiragu mnamo Desemba 27, 2023 aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba “siku chache za msimu wa sherehe za Desemba zimetuanika kama kaunti ambayo haiwezi kutekeleza ustaarabu wa ulevi wala sheria husika”.

Katika utekelezaji wa amri ya Bw Gachagua, Gavana Irungu Kang’ata alikuwa ametangaza kwamba maombi ya 2023 ya leseni za baa yalikuwa 4,647 akiapa kuzipunguza hadi 2,291.

Hata hivyo, rekodi za Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) katika kaunti hiyo zinaonyesha kwamba baa zilizokuwa zimesajiliwa na ambazo zinahudumu kwa sasa ni 5,447 kumaanisha zingine mpya 800 zilisajiliwa.

Tayari, mbunge wa Maragua Bi Mary wa Maua ameteta kwamba “msasa wa baa Murang’a ulikuwa sarakasi huku hata zilizopendekezwa kufungwa ziliishia kuidhinishwa”.

Bi Wa Maua, aidha, ameteta kwamba biashara ya mihadarati bado inavuma katika Kaunti ya Murang’a licha ya amri ya Bw Gachagua.

“Kwa mfano, katika eneo la Kiambamba biashara ya mihadarati inaendeshwa hata na maafisa wa polisi hasa wale wa jela,” akasema.

Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu alisema kwamba licha ya kuwa vita dhidi ya ulevi kiholela havifai kulenga biashara halali, “Kuna mabwanyenye ambao katika nyumba zao za kifahari kumenaswa bhangi na pombe za mauti lakini hata baada ya miezi mitatu sasa ya kuambiwa wanasakwa, hawajatiwa mbaroni”.

Bw Nyutu alisema, “Washukiwa hao hawako mafichoni, na huwa wanaonekana hata kwa hafla za umma na wanatangamana hadharani na wakubwa pasipo kunyakwa”.

Aliteta kwamba kuna baa zingine ambazo zimekuwa zikitekelezewa maandamano na wenyeji na pia kuamrishwa zifungwe kwa msingi wa kuhatarisha usalama lakini kupitia mlango wa nyuma huishia kufunguliwa.

Mshirikishi wa masuala ya uhamasisho wa kijamii kuhusu uchumi wa akiba na mikopo Bi Rahab Karicha aliambia Taifa Leo Dijitali kwamba “Tuna shida kuu kwa kuwa pesa nyingi zinazidi kumezwa ndani ya uraibu wa mihadarati na ulevi”.

Alisema miji mingi Murang’a huwa na walevi ambao ni wanafunzi katika taasisi za kitaaluma “wengine wao Mjini Murang’a wakisajiliwa katika aibu ya kunengua viuno wakiwa uchi ndani ya baa kwa malipo ya pombe”.

Katika hafla ya kuadhimisha siku ya ufisadi duniani iliyoandaliwa Mjini Murang’a, Kamishna Patrick Mukuria alikiri kwamba “ulevi umekuwa tishio kubwa na unatusababishia kila aina ya shida hata katika huduma kwa umma”.

Alisema sekta ya ulevi imekuwa ikizua visa vya ufisadi eneo hilo.

Bw Mukuria na Bw Kang’ata wamekuwa wakilumbana kuhusu nani ndiye kiini cha leseni za kiholela za biashara ya vileo.

Bw Mukuria amekuwa akisisitiza kuwa leseni hutolewa na utawala wa Kang’ata, naye Kang’ata akishikilia kuwa kamati ya kiusalama ndiyo ina mamlaka kuidhinisha maduka ya vileo almaarufu Wines and Spirits na ambayo ndiyo yametajwa kuwa kero kuu.

  • Tags

You can share this post!

Daddy Owen afunguka kuhusu uhusiano wake na Charlene Ruto

Wahuni wanaochapisha vitabu feki vya CBC wanyakwa

T L