• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Walinzi warejeshwa kwa makazi ya Mama Ngina Kenyatta

Walinzi warejeshwa kwa makazi ya Mama Ngina Kenyatta

NA CHARLES WASONGA

SERIKALI imerejesha maafisa wa usalama katika makazi ya mamake Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, Mama Ngina Kenyatta saa kadhaa baada ya kuwaondoa Jumanne jioni.

Walinzi hao walirejeshwa katika makazi yake yaliyoko katika mtaa wa Muthaiga jijini Nairobi, na nyumbani kijijini Ichaweri, eneobunge la Gatundu Kusini katika Kaunti ya Kiambu na biashara zake za kibinafsi.

Maafisa hao kutoka kitengo cha maafisa wa polisi wa kupambana na fujo (GSU) na Polisi wa Utawala (AP) walikuwa wameondolewa kutoka makazi hayo bila sababu yoyote.

Aidha, Mama Ngina hakuarifiwa kuhusu kuondolewa kwa walinzi hao wala sababu zilizochangia hatua hiyo.

Kufuatia hatua hiyo, familia ya Kenyatta iliwatuma walinzi wa kibinafsi kutoa ulinzi katika makazi ya Mama Ngina katika mtaa wa Muthaiga na kijijini Ichaweri na maeneo mengine ambako familia hiyo inamiliki mali.

Kuondolewa kwa walinzi hao kulitarajiwa baada ya maafisa wakuu wa serikali na wanasiasa wa muungano wa Kenya Kwanza, kudai kuwa Bw Kenyatta ndiye anafadhili maandamano ya Azimio.

Walinzi wa kibinafsi walipelekwa katika makazi ya Mama Ngina baada ya kundi linalojiita wafanyabiashara wa Nairobi kutisha kuandamana hadi Muthaiga ili kumwambia “amuonye Uhuru akome kudhamini maandamano ya Azimio yanayotuharibia biashara zetu.”

“Tutaandamana kwa amani kwa sababu haja yetu kuu ni biashara zetu ambazo zinaharabiwa na maandamano ambayo yamefadhiliwa na Uhuru,” akasema mwenyekiti wa kundi hilo Theuri Wanjiru kwenye barua kwa mkuu wa kituo cha polisi cha Muthaiga.

Hatua ya kuondolewa kwa walinzi katika makazi ya Mama Ngina imelaaniwa na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Mutahi Ngunyi na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wanunuzi Bidhaa (COFEK) Stephen Mutoro.

Jumatano, polisi na wafuasi wa Azimio walikabiliana watu hao walipojaribu kufanya maandamanano katika miji ya Nairobi, Nakuru, Kisumu, Wote (Makueni), Mlolongo (Machakos), Mombasa miongoni mwa maeneo mengine.

  • Tags

You can share this post!

Karua alaani hatua ya maafisa kuwakamata viongozi wa Azimio...

Maandamano: Jinsi polisi walivyozima mkakati wa Mwangi Wa...

T L