• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Wanafunzi walioendea slesi za ziada shuleni waadhibiwa vikali

Wanafunzi walioendea slesi za ziada shuleni waadhibiwa vikali

NA LUCY MKANYIKA

WANAFUNZI 10 wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Voi katika Kaunti ya Taita Taveta wamefukuzwa na usimamizi wa shule hiyo wakitakiwa kununua unga ngano na mafuta ya kupikia kwa kupatikana wakiendea slesi za ziada za mkate.

Kila mmoja wa wanafunzi hao anatakikana kununua bandali ya unga wa ngano na lita 10 za mafuta ya kupikia.

Mzazi mmoja aliambia Taifa Leo alilazimika kutumia Sh4600 kununua unga ngano na mafuta na Sh1500 akatumia kama nauli yake na mwanawe kumrejesha shuleni.

“Mwanangu alufukuzwa Jumatatu na niliporudi naye shuleni Naibu Mwalimu Mkuu alisema ni lazima tulipe na kwamba nihakikishe pia mwanangu amekamilisha kulipa karo,” akasema mama ya kijana mmoja wa waliofukuzwa.

Aidha mzazi huyo alihisi kwamba shule hiyo ililenga kuadhibu wazazi ambao kwa sasa wanatatizwa na gharama ya juu ya maisha.

“Mtoto wangu alikiri kuwa alichukua mikate zaidi ya ile inayotakikana. Maoni yangu ni kuwa angepewa adhabu mbadala,”  akasema mzazi huyo.

Alisema wanafunzi walikuwa wameanza mtihani na kamwe hakutaka mwanawe akose kuufanya mtihani huo.

Mzazi mwingine alisikitika kwamba huenda wengi wao wakakosa kufanya mtihani.

Baadhi ya wazazi na wadau wa elimu wa eneo hilo walitoa wito kwa Wizara ya Elimu kuchukua hatua dhidi ya shule hiyo huku wengi wakishangaa kuhusu adhabu kama hiyo wakati wazazi wanakabiliwa na changamoto za kifedha zilizosababishwa na gharama kubwa ya maisha.

Mwakilishi wa wazazi kwenye masuala ya usimamizi shuleni humo, Elias Mberi, alisema uamuzi huo ulitokana na mkutano uliolenga kuhakikisha wanafunzi wanafuata utaratibu uliowekwa shuleni na wanadumisha nidhamu.

“Bila shaka sasa mzazi anayegharimika atamsisitizia mwanawe umuhimu wa kuwa na nidhamu bora,” akasema Bw Mberi.

Haya yanajiri huku shule nyingi nchini zikishutumiwa kwa kuweka kanuni za kuwanyanyasa wazazi kwa kuwaamuru kulipa ada zisizo za kimsingi wakati watoto wao wamefanya makosa shuleni.

“Adhabu kama hii ya shule ya Voi haifuati sheria. Ikiwa mwanafunzi amefanya makosa madogo, aadhibiwe shuleni na sio kufukuzwa nyumbani na vilevile kuamuriwa kurudi na unga na mafuta,” akasema Bw Charles Mwadime.

Mkurugenzi wa elimu wa kauti hiyo Bw Khalif Hirey alisema kuwa ataanzisha uchunguzi dhidi ya madai hayo.

Aliwataka wazazi wa wanafunzi hao kuripoti kisa hicho kwa afisi yake ili hatua kuchukuliwa.

  • Tags

You can share this post!

Macho kwa Japan, Uhispania Kombe la Dunia la Wanawake...

Buriani: Mwanahabari Elizabeth Merab azikwa nyumbani Lwala

T L