• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 12:44 PM
Wiki ya Ubunifu nchini kuanza Desemba 6

Wiki ya Ubunifu nchini kuanza Desemba 6

NA WANGU KANURI

SERIKALI imewaomba wabunifu na washikadau katika sekta ya teknolojia kushiriki katika Wiki ya Ubunifu nchini ambayo itafanyika kuanzia Desemba 6 hadi Desemba 10, 2021 eneo la Lower Kabete, Nairobi.

Rais Uhuru Kenyatta kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, alieleza kuwa ubunifu ni injini inaoendesha ujasiriamali na kufungua nafasi za ajira kwa vijana.

Isitoshe, Rais Kenyatta alisisitiza kuwa sharti washikadau wa elimu waendelee kuboresha elimu ya teknolojia ya sayansi, ubunifu na ujasiriamali.

“Ni dhahiri kuwa tunafaa kuhakikisha kuwa kuna ushirikiano kati ya taasisi zetu na sekta mbalimbali za ubunifu nchini. Tunafaa mtaji utakaokuza mawazo haya geni ambayo yanaweza kusaidia nchi au hata ulimwengu siku zijazo,” akaeleza.

Waziri wa Elimu, Profesa George Magoha kwa upande wake alisisitiza kuwa wiki ya ubunifu itasaidia kugeuza mwelekeo wa elimu na utafiti pamoja na kuimarisha maendeleo katika taasisi na kustawisha jamii na uchumi.

Wiki hiyo ya ubunifu itajumuisha mikutano minne ya; ubunifu unaoegemea ujuzi na talanta, teknolojia na mabadiliko kwa viwanda, biashara na uanzilishaji.

Mwenyekiti wa Shirika la Ubunifu nchini (KeNIA), Dkt Tonny Omwansa akizungumza kwenye mkutano wa washikadau uliofanyika katika hoteli ya Capital Club jijini Nairobi, aliwarai wabunifu kuonyesha bidhaa na huduma walizounda.

“Wiki hii ya ubunifu itawafaa wabunifu na wanaweza wavutia watega-uchumi, washiriki au hata wateja. Tunawaomba wote walio na bidhaa na huduma walizobuni waje wazionyeshe,” akasema.

Isitoshe, Bw Omwansa alisema kuwa wiki ya ubunifu itakuwa ikifanyika kila mwaka.

“Baada ya kila mwaka, tutakuwa tukitathmini maendeleo yaliyofanywa na kujitolea kufikia matarajio yatakayoorodheshwa mwaka ujao,” akaongeza.

Balozi Simon Nabukwesi, Katibu anayesimamia Elimu ya Juu na Utafiti katika Wizara ya Elimu alisema kuwa hafla ya wiki ya ubunifu inapaswa kuwavutia watu kutoka mataifa yaliyopiga hatua za maendeleo.

“Nimewaalika watu kutoka nchi tofauti lakini ombi langu ni kwamba wiki ya ubunifu nchini Kenya iwe hafla itakayowavutia watu kutoka mataifa mbalimbali ili tuweze kusoma na kuongozwa na mataifa yaliyopiga jeki maendeleo,” akaongeza.

Kutoka kushoto: Dkt Tonny Omwansa, Florence Kimata, Sheena Raikundalia na Philip Thigo mafaisa ambao wataongoza mikutano ya uvumbuzi unaoegemea ujuzi na talanta, teknolojia na mabadiliko kwenye viwanda, biashara na uanzilishaji. PICHA/ WANGU KANURI

Mwenyekiti katika bodi ya KeNIA, Profesa Reuben Marwanga alieleza kuwa Kenya ikizidisha ubunifu itaweza kutajirika kwani ubunifu huleta huduma na bidhaa geni, nafasi za ajira na kupunguza umaskini nchini.

“Sisi kama KeNIA tungependa kuiona Kenya ikiwa imepewa cheo cha juu katika Fahirisi ya Kimataifa ya Ubunifu (GII). Hicho ni kielelezo cha maendeleo kwa nchi,” akaeleza Prof Marwanga.

Bi Sheena Raikundalia, Mkurugenzi wa Kitovu cha Teknolojia cha Uingereza nchini Kenya, alieleza kuwa wiki ya ubunifu itawapa motisha Wakenya na kuwawezesha kuwa na ujuzi wa ubunifu.

Isitoshe, Bi Sheena alipigia debe mtaala wa CBC akisema kuwa mtaala huo utawaongoza wanafunzi katika ubunifu.

“Ubunifu hulenga kusuluhisha matatizo yanayowakumba wananchi na kupanua udijitali. CBC ina mwelekeo kwa kufanikisha matakwa hayo.

“Hata hivyo, mtaala huo ili uwafae wanafunzi lazima utekelezwe kwa njia inayofaa,” akasema Bi Sheena ambaye atakuwa kiongozi wa mkutano wa ujuzi na talanta kwenye wiki ya ubunifu.

Bi Florence Kimata, Mtaalamu wa Mageuzi ya Kibiashara katika Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maendeleo ya Maeneo, alishinikiza kuwa lengo lao kama washikadau wa wiki ya ubunifu ni kuwasaidia kijumla wabunifu.

Usaidizi huu wa kijumla unalenga kuwaunganisha wabunifu na shirika za kibiashara, kuwapa mtaji wanaotaka, kuwaongoza na kuwashirikisha na wateja, viwanda na vituo vya utafiti pamoja na kuwawezesha kuwa huru katika biashara zao.

Isitoshe, Bi Kimata alieleza kuwa wiki ya ubunifu itawafaa sana Wakenya wote kutoka kaunti zote 47.

“Tumeshirikiana na viongozi kutoka kaunti mbalimbali na taasisi zote nchini na tumewaeleza wawarai Wakenya waliobuni bidhaa au huduma spesheli na za kipekee wazilete kwenye wiki ya ubunifu ili tuweze kuziona na kuwasaidia,” akaeleza.

Wiki ya ubunifu itawaleta pamoja wakuu kutoka serikali za kaunti, sekta binafsi, washiriki wa maendeleo, wanaounda sera, wanahabari na jamii kwa jumla ili kuwafaa Wakenya.

Dhima ya Wiki ya Ubunifu ni kuonyesha ubunifu wa Wakenya na pia kuendeleza miradi ya nchi chini ya Ajenda Nne Kuu na Ruwaza ya 2030.

You can share this post!

TAHARIRI: Magavana walipe madeni ya kaunti

Naomba unikome!

T L