• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 8:50 AM
Naomba unikome!

Naomba unikome!

Na MARY WANGARI

KISANGA cha mapenzi kugeuka shubiri kati ya Gavana wa Machakos Alfred Mutua na Bi Lilian Nganga, kimechukua mkondo mpya huku Bi Nganga akimtaka Dkt Mutua akome kumng’ang’ania na aendelea na maisha yake.

Akizungumza na waandishi habari Alhamisi jijini Nairobi, Bi Nganga alilalamika kuwa, licha ya kudhihirisha kwamba hana hisia zozote kwa mpenziye wa awali, Bw Mutua angali hajakubali kwamba wametengana.

“Tulipokutana Windsor Golf and Country Club mnamo Septemba 22, 2021, tukiwa pamoja na marafiki zetu wawili na baada ya visa viwili vya uhalifu, nilimsihi tuachane kiutu uzima, kwa amani na nikamkumbusha kwamba hata hatukuwa tumeoana. Bw Mutua kwa hasira alinitaja kama adui wake nambari moja na kutishia kuniponda hadi niwe ‘majivu’. Aliapa kunipokonya kila kitu nilicho nacho na ninachomiliki. Tayari hayo yameanza kujitokeza kwa kuwa ameniagiza kumrejeshea pesa zote alizowahi kunipa au nilizowahi kutumia,” Bi Nganga alisimulia.

Alisema gavana huyo alitishia pia kuwadhuru washirika wake na kumwagiza aombe msamaha na kuondoa jumbe alizochapisha mitandaoni kuhusu kutengana kwao.

Alieleza kuwa licha ya kukatiza uhusiano wa kimapenzi kati yao mapema Juni 2021, mkuu huyo wa Kaunti ya Machakos amekuwa akisema magazetini na mitandaoni kuwa wangali marafiki na waliachana kwa amani, akirejelea matamshi ya gavana huyo wiki mbili zilizopita.

Bi Nganga sasa amemsihi Inspekta Mkuu wa Polisi, Hillary Mutyambai, na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Noordin Haji, kuingilia kati akisema anahofia usalama wake.

“Namsihi Inspekta Mkuu wa Polisi na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kuharakisha uchunguzi dhidi ya Mutua na kumshtaki kwa makosa aliyotekeleza kufikia sasa kabla ya kunidhuru pamoja na marafiki zangu,” akasema.

Alimtaka Bw Mutua kukoma kumhangaisha kisaikolojia na kiuchumi hali aliyotaja kama dhuluma za kijinsia.

Isitoshe, alishutumu aliyekuwa mpenziwe dhidi ya kumpokonya mali kwa njia haramu ambayo ni pamoja na gari la kibinafsi na asilimia 90 ya hisa za kampuni yake binafsi.

Alieleza jinsi Bw Mutua alivyoghushi saini kabla ya kuhamisha hisa za Bi Nganga katika Ndash Enterprises LTD, na kumpa dada yake Anne Mbandi Mutua, akisema tayari ameandikisha ripoti katika Kituo cha Polisi cha Kilimani.

“Mnamo Septemba 8, 2021, Bw Mutua akiandamana na mlinzi wake ambaye ni afisa wa polisi, Martin Nzinghi, aliwasili kwenye maegesho ya gari nyumbani kwangu Kileleshwa, Nairobi, na bila mimi kujua wala ruhusa kutoka kwangu, na kwa kutumia ufunguo aliokuwa amepata kwa njia haramu, wakaondoka na gari langu la kibinafsi lenye nambari ya usajili, KBY 186G, lililokuwa limesajilishwa kwa jina langu tangu 2014. Mutua kisha alihamisha umiliki wa gari hilo, akaliweka kwa jina lake, na kuliuza kwa mtu mwingine. Niliwasilisha kesi inayoendelea kortini hivyo sitajadili zaidi, ila kumpa notisi aliyenunua kuwa ningali mmiliki wa gari hilo,” akaeleza.

Aidha, alimshutumu Bw Mutua dhidi ya kueneza porojo dhidi yake ikiwemo kwamba anatumia mihadarati na ni kibaraka wa Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka na Gavana Kivutha Kibwana (ambaye ni mjombake Gavana Mutua) wanaomtumia kumwangusha kisiasa Gavana Mutua.

“Namwagiza hadharani Bw Mutua arejeshe mali yangu mara moja, akome kutishia maisha yangu na wanaonizingira na aache kiburi, matumizi mabaya ya mamlaka na unyanyasaji. Anahitaji kusonga mbele na maisha yake,” akasema.

You can share this post!

Wiki ya Ubunifu nchini kuanza Desemba 6

Wahalifu mtandaoni kuchukuliwa hatua – Matiang’i

T L