• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Wito hazina ya kitaifa ya mashujaa ianzishwe

Wito hazina ya kitaifa ya mashujaa ianzishwe

NA TITUS OMINDE

WAZALENDO maarufu katika nyanja mbalimbali wametoa wito wa kuanzishwa kwa Hazina ya kitaifa kwa Mashujaa ili kusaidia ustawi wa mashujaa na mashujaa wa nchi kwa ujumla.

Wakizungumza mjini Eldoret mnamo Jumanne wakati wa kongamano la mashauriano la Baraza la Kitaifa la Mashujaa wa Kenya, wazalendo hao shupavu kutoka nyanja mbalimbali za umaarufu wametoa changamoto kwa serikali ya Kenya Kwanza kutekeleza ombi lao kabla ya maadhimisho ya Siku ya Mashujaa mnamo Oktoba 20.

Wakiongozwa na aliyekuwa mwanariadha wa kimataifa Janeth Jepkosgei almaarufu Eldoret Express, magwiji hao wamesema ni wakati mwafaka kwa serikali kuanzisha hazina hiyo ya kuwaenzi mashujaa kwa kuhakikisha kwamba wanafurahia kustaafu na maisha ya uzeeni kwa njia ya kifahari.

Bi Jepkosgei amesema hazina hiyo itachangia pakubwa katika kupunguza mateso kwa wale ambao wamechangia pakubwa umaarufu wa Kenya.

“Kama nchi, tunahitaji kuwa na hazina itakayosaidia mashujaa wetu katika uzee wao. Wengi wa mashujaa wetu huishia kuishi katika hali ya ufukara kwa kukosa usaidizi wa kifedha wa kutegemewa,” akasema Bi Jepkosgei.

Bi Jepkosgei amepongeza serikali kwa kuanzisha Baraza la Kitaifa la Mashujaa akibainisha kuwa baraza hilo litatumika kama jukwaa la mashujaa na mashujaa kutatua changamoto zao na kuleta suluhu mwafaka.

Amesisitiza umuhimu wa mfuko huo kuhudumia mashujaa wote kutoka nyanja mbalimbali bila kujali umri wao.

Aidha ameongeza kuwa makundi yote mawili ya mashujaa yanahitaji kuungwa mkono na serikali ili kuitumikia nchi kwa njia bora zaidi.

Naibu mkurugenzi wa baraza la Kitaifa la Mashujaa Dkt David Mbuthia amesema serikali tayari imeanza mipango ya kuanzisha hazina hiyo.

Dkt Mbuthia amesema baraza lake linashirikiana na wadau wote kupitia mikutano ya wadau mbalimbali ili kukusanya maoni ya jinsi ya kufanya maisha ya mashujaa wote kuwa bora zaidi.

Amesema tangu kuanzishwa kwa baraza hilo kupitia sheria ya Mashujaa wa Kenya ya mwaka 2014 mengi yamefanyika ili kuboresha ustawi wa mashujaa.

“Wito wa kuanzisha hazina ya mashujaa tayari umeshughulikiwa kupitia sheria hiyo ambayo kwa Kiingereza ni Kenya Heroes, 2014. Serikali imejitolea kuwasaidia mashujaa wetu kwa kila njia,” amesema Dkt Mbuthia.

Dkt Mbuthia amesema tangu mwaka 2020 baraza hilo limekuwa likifanya kazi na wadau wote kwa lengo la kubuni mbinu sahihi za kutambua mashujaa wote mbali na kuwapa uwezo wa kujikimu kimaisha.

“Tuna takriban kategoria 14 za mashujaa na tunataka kila mmoja wa mashujaa hawa asaidiwe kufikia yaliyo bora kwa nchi na ustawi wao pia,” alisema Dkt Mbuthia.

Dkt Mbuthia amesema kwa sasa baraza lake linazunguka nchi nzima kupata takwimu sahihi za mashujaa wote na kuandaa mpango ya kuwatambua kama wazalendo.

  • Tags

You can share this post!

Warembo wa Gatura wajiimarisha kwa mchezo wa karate

Hisia mseto Kenya ikianza kusafirisha samaki hadi nchini...

T L