• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
Wito wa utangamano na amani Rais Ruto akizuru Lamu

Wito wa utangamano na amani Rais Ruto akizuru Lamu

NA KALUME KAZUNGU

RAIS William Ruto amewasili mjini Mokowe, Kaunti ya Lamu kuzindua miradi ya maendeleo, ziara ya kiongozi wa nchi katika ukanda wa Pwani ikitarajiwa kuendelea hadi Jumapili.

Dkt Ruto ametoa wito wa amani na utangamano nchini, akisema kipindi cha uchaguzi kilishapita na kwa sasa lengo lake ni kuhakikisha serikali ya Kenya Kwanza inafanyia Wakenya maendeleo.

“Lengo langu ni kushirikiana na viongozi kwa manufaa ya nchi na kufanikisha miradi ya maendeleo,” amesema Dkt Ruto.

Amesema njia ya pekee ya kuleta uwiano na usawa nchini ni kupitia jamii kuelimishwa, akitaja kuwa Sh630 bilioni zimetengewa masuala ya elimu kuona kwamba watoto wote, wa maskini na tajiri, wanapata elimu ya kutosha ili kujiendeleza kimaisha.

Wakati wa ziara hiyo, Spika wa Lamu Azhar Mbarak, ambaye ni mwanachama wa Orange Democratic Movement (ODM) na mrengo wa Azimio La Umoja-One Kenya, amemuomba Rais Ruto kuwasamehe kwa yaliyotokea kufuatia maandamano nchini.

Bw Mbarak amesema yuko tayari kuzungumza na kiongozi wa Azimio Raila Odinga ‘Baba’ ili asitishe maandamano.

Amesema kuwa hata wananchi wamechoka kurushiwa vitoa machozi na hata wanapofuka kutokana na athari za maandamano.

Gavana wa Lamu Issa Timamy amesema katu Lamu haijawahi kushiriki maandamano hayo yaliyoitishwa na Azimio.

“Lamu haitaonekana kwenye maandamano hata siku moja,” amesema gavana huyo akifafanua kwamba watu wa Lamu wameelekeza fikra zao kwenye kilimo, uvuvi, utalii na maendeleo mengineyo badala ya kushiriki maandamano na uharibifu wa mali.

Gavana Timamy amesema wakulima Lamu wamekuwa wametia bidii zaidi badala ya kujihusisha na maandamano na kuvalia sufuria kichwani, hivyo mwaka huu 2023 wako tayari kuvuna pakubwa.

Naye Waziri wa Masuala ya Umma Aisha Jumwa amewapongeza pakubwa wakazi wa Lamu kwa kujiepusha na maandamano akiwasisitizia haja ya kuangazia maendeleo na amani.

Mbali na Lamu, Rais Ruto leo Alhamisi pia atazuru mji wa Ngao, eneobunge la Garsen, kaunti ya Tana River ambapo atakabidhi jamii ya wavuvi hundi na kisha kuzindua mradi wa unyunyizaji maji mashambani wa TARDA eneo hilo.

Ijumaa, Rais Ruto atakuwa katika Kaunti ya Kilifi kabla ya kufika Kaunti ya Mombasa Jumamosi.

Jumapili atakamilisha ziara yake Ukanda wa Pwani kwa kuzuru Kaunti ya Kwale.

  • Tags

You can share this post!

Soccer Assassins wawanyoa Solasa Queens bila maji

Mradi wa mabohari wa The Link kusaidia kuimarisha uchumi

T L