• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Wito wakazi wachague wanasiasa waadilifu

Wito wakazi wachague wanasiasa waadilifu

Na KENYA NEWS AGENCY

VIONGOZI wa kidini katika Kaunti ya Laikipia, wametoa wito kwa wapiga kura kuwachunguza wanasiasa watakaowania nyadhifa mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa 2022 kabla ya kuwachagua.

Kupitia muungano wao wa Dini uliobandikwa jina la ‘Dialogue Reference Group’, viongozi hao, Jumatano, walisema kuwa wananchi wanapaswa tu kuwachagua wanasiasa ambao wameonyesha uadilifu.Katika kikao na wanahabari mjini Nanyuki, walibaini kuwa baadhi ya wanasiasa wanafanya kazi ya kuwatusi wapinzani wao na kuwanunulia vijana pombe duni za bei za chini ili kuwashangilia kwenye kampeni zao badala ya kuuza ajenda zao.

Askofu Francis Maina wa Kanisa la Gospel Outreach, alisema wanasiasa hao hawashughulikii masuala yanayowaathiri wananchi kama vile ujenzi wa barabara, kusuluhisha migomo ya madaktari na dawa katika hospitali za umma.“Tuna matatizo makubwa yanayoathiri watu wetu ambayo yanahitaji kushughulikiwa.

Wagonjwa wanatafuta matibabu katika vituo vya afya nje ya Laikipia jambo ambalo si zuri,” alisema Askofu Maina.Kadhalika, aliwaonya wanasiasa kuepuka maneno yanayochochea chuki na kuleta uhasama kati ya watu.Kwa upande wake, Askofu Raphael Mwiti alibainisha kuwa visa vya ukosefu wa usalama vinavyotokana umiliki haramu wa bunduki vimekithiri katika baadhi ya maeneo ya Laikipia, Baringo, Isiolo na Marsabit.

“Tunataka Serikali ya Kitaifa iangazie suala hili na ikiwezekana iwakamate na kupiga marufuku umiliki wa silaha. Nchi hii ni yetu na hatuna pa kwenda,” akasema Askofu Mwiti.Alisema serikali inapaswa kuhakikisha kuwa wanaomiliki silaha wana leseni na zinapaswa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Naye, mwakilishi wa Wanawake wa Baraza la Kitaifa la Makanisa nchini (NCCK), Susan Kamiru alisema kuwa serikali inafaa kuwateua maafisa wa polisi ambao watakuwa wakishughulikia masuala ya unyanyasaji wa kijinsia hasa dhidi ya wanawake.Bi Kamiru alibainisha kuwa wanawake wananyanyaswa kwa njia nyingi, hasa wakati wa uandalizi wa uchaguzi.

“Wanawake wanaotoka katika maeneo ambayo watu wanapigana hupitia dhuluma mbalimbali. Hao wanafaa kulindwa. Hata hivyo, tunatoa wito kwa wanawake wapige ripoti pindi tu wanapodhulumiwa,” akasema Bi Kamiru.Kwingineko, Kamishna wa Kaunti ya Tana River, Mbogai Rioba, amewataka wakazi kujitahidi kudumisha amani iliyopo, ili kuvutia wawekezaji zaidi katika eneo hilo.

Akizungumza na wanahabari, Bw Rioba alishukuru jamii za wafugaji na wakulima wanaoishi katika eneo hilo, kwa kudumisha amani.“Ninaendelea kusisitiza kuwa tunafaa kudumisha amani kila wakati. Tukidumisha amani, uchumi wetu utaendelea kuimarika.

Tunahitaji watu wengi zaidi kuja kuwekeza ili vijana wa eneo hilo wapate nafasi za ajira,” akasema Bw Rioba.Alisema kuwa kwa miaka mingi ukame umekuwa kichocheo cha migogoro, kuwakutanisha wafugaji wandani na vikundi vya wakulima, huku wakihangaika kutafuta rasilimali chache, lakini hali inaonekana kubadilika na kuwa nzuri.

Aidha aliwashauri wazazi kuwekeza katika elimu ya watoto wao jambo ambalo kwa muda mrefu litachochea maendeleo katika eneo hilo.Gavana wa Kaunti hiyo, Dhadho Godhana, aliunga mkono maneno hayo huku akisisitiza kuwa udumishaji wa amani ni jambo muhimu sana katika ukuaji wa uchumi.

“Wakati huu hamjapigana, wanachama wa jamii za Orma na Pokomo, sasa wamekuwa na hekima zaidi, wakichagua kutatua matatizo yao kama watu wazima” akasema gavana huyo.Kwa upande wake, Seneta wa eneo hilo, Juma Wario, aliwasihi wapiga kura kutowapigia kura viongozi kwa misingi ya kikabila, kidini au kiukoo, bali kutokana na uwezo wao wa kuwaleta watu pamoja.

You can share this post!

Timu ya voliboli ya ufukweni ilivyong’ara hadi...

Lusaka asifu uongozi wa wanawake

T L