• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
Timu ya voliboli ya ufukweni ilivyong’ara hadi Olimpiki

Timu ya voliboli ya ufukweni ilivyong’ara hadi Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE

KENYA ilifanya vizuri zaidi kuliko matarajio yake kwenye voliboli ya ufukweni mwaka 2021.

Kwa mujibu wa kocha mkuu wa timu ya kinadada ya voliboli ya ufukweni Sammy Mulinge, lengo la Kenya lilikuwa kufika fainali ya kipute cha Continental Cup katika kitengo cha kinadada na pia wanaume mjini Agadir, Morocco mwezi Juni.’Kwa kweli tulifanya bora zaidi kwa kutwaa taji la Bara Afrika na kujikatia tiketi ya kushiriki Olimpiki kwa upande wa kinadada,’ anasema.

Kinadada wa Kenya walipepeta Nigeria, Cape Verde and wenyeji Morocco katika kiwango hicho cha juu barani Afrika na kuingia Olimpiki kwa mara ya kwanza kabisa. Vipusa wa Mulinge walikuwa wamelemea Rwanda, Tanzania na wenyeji Uganda katika mashindano ya Zoni ya Tano mjini Entebbe kabla ya kuingia Continental Cup.

‘Ilikuwa motisha kubwa kwa wachezaji na kivutio kwa kizazi kijacho cha wachezaji,’ anasema Mulinge kuhusu kampeni ya kinadada wa Kenya, Gaudencia Makoha, Brackcides Agala, Phoscah Kasisi na Yvonne Wavinya katika Continental Cup. Aliongeza,’Wanaume waliorodheshwa nafasi ya sita barani Afrika kwa hivyo bado wana fursa ya kufanya zaidi kupata matokeo mazuri.

‘Kutokana na janga la Covid-19 na muda mchache tuliokuwa nao wa matayarisho, nitapatia Shirikisho la Voliboli Kenya (KVF) alama nane kwa 10,’ anasema. Mulinge amefichua kuwa wameweka malengo makubwa ya 2022. ‘Malengo yetu madogo ni kufuzu kushiriki michezo ya Jumuiya ya Madola mweziMachi 2022 na mashindano ya dunia ya chipukizi na watu wazima.

Tunalenga pia kuwa na timu nzuri ya Olimpiki za Paris 2024 kwa kucheza mashindano mengi ya kitaifa. Tunataka kufanya voliboli ya ufukweni iwe maarufu hapa nchini,’ anasema. Mulinge anaamini kuwa Kenya inaweza kushinda mechi katika mashindano makubwa kuliko hata voliboli ya kawaida.

Timu ya voliboli ya ufukweni, anasema, ina uwezo sawa wa kushindana na mataifa yanayofahamika zaidi kwa mchezo huu.’Kwa mfano, Gambia sasa ni miamba wa voliboli ya ufukweni duniani. Kwa hivyo, tukiongeza juhudi zetu, tunaweza kuwa bega kwa bega na mataifa yanayovuma katika voliboli ya ufukweni,’ anasema.

Mulinge anaamini kuwa voliboli ya ufukweni si ghali kumudu kwa sababu haihitaji ukumbi. ‘Tunachohitaji tu ni changarawe. Wachezaji wanaohusika ni wawili kwa timu kwa hivyo haigharimu fedha nyingi,’ anasema kabla ya kufichua kuwa tatizo kubwa ni mtazamo kuwa voliboli ya ufukweni ni ya wachezaji wadhaifu na waliostaafu.

Agala na Makokha walishiriki Olimpiki nchini Japan na kumaliza nafasi ya pili kutoka mwisho baada ya kupoteza dhidi ya Amerika, Latvia na Brazil katika mechi za makundi katika ufuo wa Shiokaze.

You can share this post!

Nusu-fainali ya kukata na shoka

Wito wakazi wachague wanasiasa waadilifu

T L