• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
400 wafa vita kati ya Israeli na Wapalestina vikichacha

400 wafa vita kati ya Israeli na Wapalestina vikichacha

Na AFP

VITA vikali kati ya Israel na Palestina viliendelea kuchacha jana kwa siku ya nne mfululizo huku Palestina wakirusha makombora kadhaa upande wa mahasimu kama njia ya kujibu mashambulizi yaliyoanza wiki hii.

Nchi hizo ziliingia vitani mnamo Jumatatu baada Israeli kuvamia msikiti eneo la mzozo la Gaza, Mashariki mwa Jerusalem. Msikiti huo una umuhimu kwa Waislamu huku pia ikitumiwa na Wayahudi kwa ibada takatifu.

Tangu Jumatatu, vifo 83 vimetokea eneo la Gaza ambalo hujumuisha raia wengi Wapalestina na unaongozwa na wapiganiaji wa Hamas. Watu wengine saba nao walifariki upande wa Israel.

Wizara ya Afya ya Gaza nayo ilithibitisha vifo hivyo na kufichua kuwa zaidi ya watu 400 wamejeruhiwa tangu mapigano hayo yazuke mnamo Jumatatu.

Uhasama kati ya Wapalestina na maafisa wa polisi tangu mwanzo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan uliokamilika jana pia unadaiwa kuchochea mapigano hayo.

Hapo jana, vita hivyo vilikolezwa kutokana na kisa cha Jumatano ambao mwanaume wa Kiyahudi alivamiwa na mwengine Mwaarabu.

Baadaye umati wa Wayahudi ulimtoa mwanaume mwaarabu/kipalestina ndani ya gari lake kisha kumpa kichapo kikali.Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akizungumza mnamo Jumatano jioni, aliapa kwamba atafanya juhudi zote kulinda Israel akishutumu Palestina kwa uchokozi usiofaa.

Mnamo Alhamisi, majeshi ya Israel (IDF) yalithibitisha kwamba makombora 1,500 yalikuwa yamerushwa kutoka Gaza yakilenga miji mikuu inayopatikana Israel.

Huku vita vikiendelea kuchacha kati ya nchi hizo jirani na hasimu, viongozi mbalimbali ulimwenguni wametoa wito kwa nchi hizo zikumbatie utulivu.

Rais wa Marekani Joe Biden ni kati ya viongozi ambao walishutumu ghasia hizo na kusema kwamba anaunga mkono upande wa Israel. “Nina matumaini kwamba ghasia hizo zitaisha. Hata hivyo, Israel ina kila haki ya kujilinda kutoka kwa maelfu ya kombora yanayorushwa kutoka upande wa Gaza,” akasema Rais Biden katika ikulu ya White House.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Kimataifa Antonio Guterres alisema wamekutana kujadiliana kuhusu ghasia hizo lakini bado UN haijatoa taarifa rasmi kuhusu msimamo wake.

You can share this post!

Kilio Taveta usimamizi wa shamba la Ruto ukikausha Ziwa Jipe

DPP aagizwa kufichua ushahidi wa kesi ya ufisadi dhidi ya...