• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 11:39 AM
Hamas yasema haitaachilia mateka wa Israel mpaka vita vikome

Hamas yasema haitaachilia mateka wa Israel mpaka vita vikome

NA MASHIRIKA

MOSCOW, URUSI

AFISA wa Hamas amesema kundi linalotawala Gaza halitaachilia huru waliotekwa hadi makubaliano ya kusitisha mapigano yatakapokubaliwa.

Hii ni kwa mujibu wa gazeti la Kommersant la Urusi.

Gazeti hilo limemnukuu afisa mmoja aitwaye Abu Hamid akisema siku ya Ijumaa, Oktoba 27, 2023 kwamba kundi hilo linahitaji muda kuwatambua wale wote waliotekwa nyara huko Gaza na makundi mbalimbali ya Wapalestina wakati wa shambulizi lililoongozwa na Hamas dhidi ya Israeli Oktoba 7, ambalo lilichochea vita hivyo.

Abu Hamid, alinukuliwa akisema kwamba Hamas ilipanga kuwaachilia huru waliotekwa nyara ila Israeli imekataa kusitisha mapigano.

“Mamia ya raia na wapiganaji kutoka makundi mbalimbali ya Wapalestina waliingia katika maeneo yaliyomilikiwa kimabavu mwaka 1948, na kuwateka makumi ya watu – wengi wao wakiwa raia,” akasema Hamid.

“Tunahitaji muda kuwatambua wote waliotekwa katika Ukanda wa Gaza na kisha kuwaachilia,” afisa huyo aliongeza.

Abu Hamid pia alisema kuwa mashambulizi ya anga ya Israeli huko Gaza yamewaua mateka 50.

Akiripoti kutoka Moscow, mwandishi wa habari Yulia Shapovalova alisema ziara ya wajumbe wa Hamas kwa kiasi kikubwa ilionekana kama jaribio la Urusi kutangaza kwamba haijasimama na kikundi fulani kwenye mzozo huo.

Moscow inataka kuonyesha kwamba inabakia kigogo kwa kukutana na wawakilishi wa Hamas na kujaribu kupatanisha pande zote mbili.

Pia alisema kuna matumaini kwamba mkutano ambao ulifanyika kati ya maafisa wa Urusi, Iran na Hamas huenda ukafanya watu watatu waliotekwa kuwachiliwa.

Watatu hao walikuwa na pasipoti za Urusi.

Shapovalova aliongeza kuwa Hamas haikutoa maoni yoyote kuhusu uwezekano wa kuwaachilia mateka wengine.

Zaidi ya mateka 200 wanazuiliwa na Hamas katika Ukanda wa Gaza baada ya kukamatwa wakati wa mashambulizi ya kundi la Wapalestina Oktoba 7, kulingana na Israeli.

Hamas siku ya Jumatatu iliwaachilia huru wanawake wawili wakongwe wa Israeli kutoka katika eneo lililozingirwa.

Juhudi za upatanishi kati ya pande hizo mbili kuhusu mateka hao zinaongozwa na Misri na Qatar.

Zaidi ya Wapalestina 7,000 wakiwemo watoto wasiopungua 2,913 wameuawa katika mashambulizi ya Israeli yaliyolenga Gaza tangu Oktoba 7.

Israeli imezuia upatikanaji wa vifaa muhimu Gaza, ikiwa ni pamoja na mafuta, huku ikitekeleza mashambulizi ya mabomu ambayo yameharibu vitongoji kadhaa na kufanya upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kuwa ngumu.

Wakati uo huo, Umoja wa Mataifa umeonya kuwa huenda watu wengi zaidi wakapoteza maisha yao kweye mzozo huo.

“Watu wanakufa Gaza, sio tu kwa sababu ya mashambulizi ya mabomu bali kwa sababu wamekosa chakula na misaada kama vile ya matibabu,” UN ulisema.

  • Tags

You can share this post!

KNEC yasema imezima mianya yote ya wizi wa mitihani ya KCPE...

Kaunti kupokea malalamishi ya wagonjwa moja kwa moja...

T L