• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Hofu vimbunga vikiua watu 100

Hofu vimbunga vikiua watu 100

Na MASHIRIKA

NEW YORK, Amerika

RAIS Joe Biden wa Amerika ameahidi kuyasaidia majimbo yaliyoathiriwa na msururu wa vimbunga Jumapili, ambapo viliharibu mamia ya nyumba, biashara na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 100.

Akitaja vimbunga hivyo kama “mojawapo ya mikasa mikubwa zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo”, Biden aliidhinisha msaada wa dharura kutolewa kwa jimbo la Kentucky, ambako karibu watu 22 wanakisiwa kufariki.

Jimbo hilo ndilo limeathiriwa zaidi na vimbunga hivyo.

“Ni mkasa mkubwa. Hadi sasa, hatujui idadi kamili ya watu ambao wamefariki na kiwango cha uharibifu ambacho kimefanyika,” akasema Biden, akionekana mwenye hofu.

Akaongeza: “Natoa ahadi kwenu kwamba tutatoa msaada wowote utakaohitajika. Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kwamba waathiriwa wamepata msaada huo.”

Miongoni mwa maeneo yaliyoharibiwa ni kiwanda cha kutengeneza mishumaa cha Mayfield, jimboni Kentucky.

Vimbunga pia viliharibu hospitali katika eneo la Arkansas na kuwaua wafanyakazi sita katika ghala moja jimboni Illinois.

Gavana Andy Beshear wa Kentucky alisema uharibifu huo ndio mkubwa zaidi kuwahi kutokea katika jimbo hilo.

Alisema kuwa karibu wafanyakazi 40 waliokolewa katika kiwanda hicho, ambapo wafanyakazi 110 walikuwa ndani wakati mkasa huo ulipotokea.

“Itakuwa kama muujiza ikiwa tutampata mtu mwingine akiwa hai,” akasema Beshear.

“Sijawahi kuona uharibifu mkubwa kama huu. Nimeishiwa na maneno kutaja hali hii. Kuna uwezekano idadi ya maafa hapa ikapita zaidi ya watu 100,” akasema Beshear kwenye kikao na wanahabari.

Video na picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha majengo katika eneo la Mayfield yakibomoka huku mawe na matofali yake yakiangukia magari yaliyokuwepo.

Mkuu wa Kikosi cha Kuzima Moto katika eneo hilo, Jeremy Creason, alisema kiwanda hicho cha mishumaa “kiliharibiwa kabisa.”

Makao ya kikosi hicho pia ni miongoni mwa maeneo yaliyoharibiwa.

Mfanyakazi mmoja katika kiwanda hicho aliomba msaada kupitia njia ya mtandao wa Facebook.

“Tumekwama. Tafadhali tusaidieni,” akasema mfanyakazi huyo, kwenye video aliyopeperusha moja kwa moja.

Wafanyakazi wenzake walisikika wakilia huku wakiomba msaada.

“Tuko katika kiwanda cha kutengenezea mishumaa, Mayfield. Tafadhali tuombeeni,” akasema.

Mwanamke huyo alitambuliwa kama Kyanna Parsons-Perez.

Kwenye mahojiano na kituo cha televisheni cha NBC, alisema tukio hilo lilikuwa la kuhofisha sana.

“Sijawahi kujikuta katika hali hiyo mashani mwangu. Sikudhani kama ningefanikiwa kutoka nikiwa hai,” akasema.

Miongoni mwa wafanyakazi ambao wameripotiwa kutoweka ni Janine Denise, 50, ambaye ni mama wa watoto wanne.

“Ni msimu wa Krisimasi. Huwa anafanya kazi katika kiwanda hicho ambapo huwa anatengeneza mishumaa kama zawadi kwa watu. Hatujasikia lolote kufikia sasa. Sitaki kufanya maamuzi yoyote ijapokuwa matumaini yetu yanaendelea kudidimia,” akasema.

Vimbunga hivyo vinadaiwa kusababishwa na upepo mkali na ngurumo kadhaa za radi zilizotokea Jumamosi usiku kaskasini mashariki mwa jimbo la Arkansas.

Vimbunga hivyo baadaye vilielekea kutoka jimbo hilo hadi katika majimbo ya Missouri, Tennessee na Kentucky.

Kituo cha Kitaifa cha Kutabiri Hali ya Hewa (NWSSPC) kilisema kilipokea ripoti 36 kuhusu vimbunga hivyo katika majimbo ya Illinois, Kentucky, Tennessee, Missouri, Arkansas na Missisippi.

Hali hiyo inadaiwa kuchangiwa na viwango vya juu vya joto na unyevunyevu.

“Hili ni tukio la kihistoria. Ni hali itakayokumbukwa na vizazi kadhaa vijavyo,” akasema Victor Gensini, ambaye ni profesa katika masuala ya hewa katika Chuo Kikuu cha Northern Illinois.

You can share this post!

Uhuru asisitiza umuhimu wa umoja

Ndoto ya BBI lazima itatimizwa, Uhuru asema

T L