• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Hofu walioambukizwa Ebola UG wakifika 84

Hofu walioambukizwa Ebola UG wakifika 84

NA DAILY MONITOR

KAMPALA, UGANDA

VISA vya maambukizi ya maradhi ya Ebola vimeongezeka na kufikia 14 jijini Kampala, Uganda, baada ya watu tisa zaidi kuthibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo hatari, imesema Wizara ya Afya.

Hapo jana Jumatatu, Waziri wa Afya nchini humo, Jane Ruth Aceng, alisema kuwa watu hao wamewekwa kwenye karantini katika Hospitali ya Kitaifa ya Mulago.

Alisema watu hao waliambukizwa na watu waliothibitishwa kuwa na maradhi hayo katika wilaya ya Kassanda.

“Visa hivyo vinatokana na watu waliothibitishwa kuambukizwa katika wilaya ya Kassanda. Mmoja wa waathiriwa alifariki alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali ya Mulago,” akasema Dkt Aceng.

Tangazo la waziri huyo linajiri saa chache baada ya kusema Jumapili walikuwa wamethibitisha visa vitano.

Hii ni baada ya watu wawili zaidi kutoka hospitali ya Mulago kuthibitishwa kuugua.

Wawili hao walikuwa wamehamishiwa katika hospitali hiyo kutoka Kituo cha Matibabu ya Maradhi ya Ebola jijini Entebbe.

Waziri huyo alisema kuwa visa hivyo vipya vinajumuisha watu saba wa familia moja (ya mwathiriwa kutoka Kassanda aliyefariki) kutoka eneo la Masanafu na mhudumu mmoja wa afya aliyempeleka marehemu katika hospitali ya kibinafsi.

Mkewe mhudumu huyo pia alithibitishwa kuambukizwa.

Kulingana na wizara, visa hivyo vinafikisha idadi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa maradhi hayo kuwa 84.

Wizara ilieleza kwamba kufikia sasa, watu 28 ndio wamefariki kutokana na maradhi hayo, huku 26 wakipona.

Kisa cha kwanza cha maradhi hayo kilithibitishwa Septemba 19.

Zaidi ya hayo, wizara inafuatilia hali za watu 1, 746 wanaodaiwa kutangamana na watu walioambukizwa maradhi hayo.

Watu 19 wamelazwa katika hospitali tofauti wakiwa na maradhi hayo.

Ebola huwa inasambazwa kupitia majimaji ya mwili. Dalili zake huwa homa kali, kutapika, kuvuja damu na kuendesha.

Aina ya Ebola inayoendelea nchini Uganda inaitwa Sudan Ebola, ambapo kwa sasa haina chanjo yoyote maalum.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kuwa majaribio ya kutafuta chanjo yake yataanza katika wiki kadhaa zijazo.

Mara ya mwisho ambapo Uganda ilikumbwa na maafa kutokana na maradhi ya Ebola ilikuwa ni 2019.

Wakati huo huo, Baraza la Jiji la Kampala limetangaza namba ya simu ambayo watu watakuwa wakipiga kuripoti visa vyovyote vya Ebola.

Namba hizo ni 0800299000; namba za mtandao wa WhatsApp ni 0708970194 au 0776140454. Kupitia namba hizo, raia wanaweza pia kutafuta maelezo yoyote kuhusiana na maradhi hayo.

Baraza hilo pia limetoa ambulensi kadhaa zitakazotumiwa kuwasafirisha waathiriwa kupata matibabu.

Wiki iliyopita, Rais Yoweri Museveni alitangaza masharti ya kuingia ama kutotoka katika wilaya za Mubende na Kassanda kutokana na idadi kubwa ya maambukizi.

  • Tags

You can share this post!

Mkenya Tikolo aajiriwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya...

Mauaji ya mwanahabari Mpakistani yaibua maswali

T L