• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Idadi ya waliouawa na magaidi Nigeria yaongezeka hadi 102

Idadi ya waliouawa na magaidi Nigeria yaongezeka hadi 102

ABUJA, NIGERIA

TAKRIBAN wanachama 102 wa kikundi cha walinzi wa ndani na raia wameuawa na magaidi walioshambulia maeneo ya Kaskazini Magharibi mwa Katsina, jimbo ambalo Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari anatoka.

Majambazi hao walivamia jamii zilizo chini ya maeneo ya Guga, Kakumi, Kandarawa na Jargaba ambalo ni eneo la serikali ya mtaa wa Bakori na kusababisha hasara kubwa.

Rais Buhari ameamuru msako mkali dhidi ya magaidi hao.

Rais huyo alilaani mashambulio hayo na kusema kuwa juhudi za walinzi hao ambao wamekuwa wakikali uhalifu katika maeneo mbalimbali hazitasahaulika.

Alithibitisha taarifa za polisi kuwa majambazi hao walivamia msafara wa askari msituni walipokuwa wakienda kuiokoa mifugo iliyoibwa na majambazi hao.

“Natuma rambirambi kwa familia za waathiriwa wa shambulio hilo. Hata hivyo, tumeanza kufanya juhudi za kuwasaka waliotenda unyama huo,” akasema Rais.

Gambo Isah, afisa wa uhusiano wa polisi wa jimbo la Katsina, alitoa ripoti kuhusu mashambulizi hayo ambayo yalitekelezwa na majambazi wakitumia bunduki aina ya AK-47.

Shambulio hilo limewaacha wanajamii katika majonzi na hofu kubwa kwani wengi wanaendelea kuwaombea jamaa zao wliotekwa nyara waachiliwe.Mmoja wa viongozi wa jamii Guga, Mahadi Guga, alithibitisha kwamba miili 72 ilipatikana msituni na kuzikwa.

“Watu 102 waliuawa na bado tunaendelea kuwasaka wengine waliotekwa nyara. Isitoshe, tumezika miili 72,” akasema Guga.

“Tunaishi katika hofu na mvutano mkubwa tangu tukio hilo kutokea. Tunaomba serikali idhibiti visa kama hivyo,” akaongeza Guga.

Aidha, kiongozi huyo wa jumuiya aliitaka serikali kulinda maisha na mali za wananchi hasa wanaoishi vijijini.Alipendekeza serikali ifanye mazungumzo na majambazi hao ili amani ya kudumu ipatikane.

Serikali ya Jimbo la Katsina imeahidi kufanya uchunguzi kuhusu mauaji hayo.

Naye Ibrahim Ahmed-Katsina, mshauri maalum wa gavana wa jimbo hilo, alisema serikali pia itazisaidia familia za waathiriwa.

Msemaji wa polisi wa jimbo hilo, Gambo Isah, aliripoti kuwa operesheni nyingine zinaendelea katika maeneo yaliyoathiriwa.

Mamlaka zinaamini kuwa Katsina na maeneo mengine ya majimbo ya Kaskazini Magharibi yanashambuliwa na majambazi wa kigeni.

Takriban watu 2,322 wameuawa tangu 2022 katika eneo hilo na wengine kutekwa nyara.

Mnamo Novemba 2022, nchi hiyo iliripoti kwamba wanajeshi waliwakamata watu watano wanaoshukiwa kuwa majambazi wa kigeni katika mtaa wa Jiba katika jimbo la Katsina.

  • Tags

You can share this post!

Familia ya Joho kortini ikilalama kuchafuliwa jina

Gavana akashifu mizozo ya taasisi

T L