• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Jeshi lamhukumu Suu Kyi miaka 4 gerezani

Jeshi lamhukumu Suu Kyi miaka 4 gerezani

Na AFP

NAYPYIDAW, Myanmar

UTAWALA wa jeshi nchini Myanmar jana ulimhukumu kiongozi wa nchi hiyo aliyeng’olewa mamlakani, Aung San Suu Kyi, miaka minne gerezani, kulingana na ripoti za vyombo vya habari nchini humo.

Msemaji wa utawala huo aliliambia shirika la AFP kwamba Suu Kyi alipatikana na hatia ya uchochezi na kuvunja kanuni za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.Msemaji huyo, Zaw Min Tun, alisema kuwa kiongozi huyo alihukumiwa miaka miwili kwa kila kosa.

Aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Win Myint, pia alihukumiwa kifungo cha miaka miwili kutokana na mashtaka kama hayo. Hata hivyo, aliongeza kuwa wawili hao bado hawajapelekwa gerezani.“Watafunguliwa mashtaka mengine wakiwa wangali kule wanakokaa,” akasema bila kutoa ufafanuzi zaidi.

Wawili hao wamekuwa wakizuiliwa katika sehemu tofauti katika mji mkuu, Naypyidaw.Vyombo vya habari havikuruhusiwa kuangazia kesi dhidi ya Suu Kyi, 76, iliyoendeshwa kisiri.Vile vile, utawala huo uliwazuia mawakili wa kiongozi huyo dhidi ya kuwasiliana na wanahabari au kutoa taarifa zozote kwa umma.

Uamuzi huo ndio wa kwanza kwenye kesi kadhaa ambazo zimewasilishwa dhidi ya kiongozi huyo tangu alipopinduliwa mamlakani mnamo Februari 1.Mashtaka mengine yanayomkabili ni tuhuma za ufisadi, utoaji wa siri za serikali na ukiukaji wa sheria ya mawasiliano.

Kijumla, mashtaka hayo yote yana adhabu ya kifungo cha zaidi ya miaka 50 gerezani.Hata hivyo, Suu Kyi amekana mashtaka hayo yote.Uamuzi huo unaonekana kuwa pigo kwa kiongozi huyo, aliyetumikia kifungo cha nyumbani kwa miaka 15 chini ya utawala wa awali wa kijeshi.

Wafuasi wake wanashikilia kuwa kesi hizo hazina msingi wowote, ambapo lengo lake ni kummaliza kisiasa, huku jeshi likiendelea kujiongezea mamlaka.Tayari, nchi kadhaa zimejitokeza kukashifu hukumu hiyo.Mbunge Charles Santiago kutoka Malaysia, ambaye ndiye mwenyekiti wa Chama cha Mataifa ya Asia Kusini kuhusu Haki za Binadamu (ASEAN), alitaja hukumu hiyo kuwa “ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.”

“Tangu mapinduzi ya kijeshi yalipotokea, ni wazi kuwa mashtaka dhidi ya Suu Kyi na mamia ya wabunge wengine ni visingizio vya utawala huo kuendelea kushikilia mamlaka,” akasema Santiago, huku akiyarai mataifa ya Asia Kusini kuingilia hali nchini humo.

Mataifa kumi ya eneo hilo yamekuwa yakiendesha juhudi za kidiplomasia kujaribu kusuluhisha mzozo huo.Santiago alisema uamuzi wa jana unaonyesha “ukaidi ulio na utawala huo dhidi ya mikakati inayoendeshwa na nchi hizo kurejesha amani.”

Mnamo Aprili, pande hizo mbili zilikubaliana kuanza mazungumzo yatakayomshirikisha kila mmoja, kama njia ya kuharakisha uwepo wa mwafaka wa amani.“Kutokana na ukaidi huo, tunayarai mataifa yote ya ukanda huu kuwazuia wawakilishi wa utawala wa Myanmar kushiriki kwenye mikutano yake na kuwazuia majenerali wa kijeshi kusafiri.

Badala yake, tunayaomba kuitambua Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” akasema, akiirejelea serikali sambamba, iliyobuniwa na wabunge waliotolewa kwenye nyadhifa zao.Myanmar imekuwa ikikumbwa na msururu wa mizozo na mivutano tangu mapinduzi hayo yalipotokea.

Kufikia sasa, vikosi vya usalama vinadaiwa kuwaua watu 1,303, kulingana na mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu.Watu 354 wanaopinga utawala huo wamehukumiwa kifo au vifungo mbalimbali gerezani.Miongoni mwa watu hao ni msaidizi wa kibinafsi wa Suu Kyi, Win Htein, aliyehukumiwa miaka 20 gerezani mnamo Oktoba.

You can share this post!

TAHARIRI: Ni msimu wa Krismasi kila mmoja awe mwangalifu

Barrow kutawala kwa muhula wa 2

T L