• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 1:12 PM
Kolera: Ufunguzi wa shule waahirishwa Malawi

Kolera: Ufunguzi wa shule waahirishwa Malawi

NA ARNALDO VIEIRA

LILONGWE, Malawi

MALAWI jana Jumatatu iliahirisha kufunguliwa kwa shule za msingi na za upili kwa wiki mbili kutokana na ongezeko la visa vya ugonjwa wa kuhara na kutapika (kolera) nchini humo.

Hatua hiyo itaathiri shule zilizoko katika miji mikubwa ya Blantyre na Lilongwe, ambayo ndio imeathirika zaidi na ugonjwa huo.

Muhula mpya ulikuwa umeratibiwa kuanza leo Januari 3, 2023 lakini ongezeko la idadi ya watu wanaoambukizwa na kufa kutokana na ugonjwa huo imeilazimisha serikali kuahirisha ufunguzi huo.

Hatua hiyo inalenga kuipa serikali muda wa kupambana na ugonjwa huo kabla ya shule kuruhusiwa kurejelea shughuli za masomo.

“Kwa wanafunzi wengine katika maeneo ambayo hayajaathirika zaidi na kolera, maafisa wa utawala wanashauriwa kuhakikisha kuwa masharti ya kuzuia kuenea kwa kolera yanazingatiwa. Miongoni mwa masharti hayo ni utoaji chanjo kwa watu ambapo hawajapewa kinga hiyo,” jopokazi la rais kuhusu corona na kolera lilisema kupitia taarifa iliyotolewa Jumatatu.

Katika ripoti ya hivi punde kuhusu hali ya kolera nchini Malawi, serikali inasema kuwa jumla ya watu 410 wamekufa kutokana na ugonjwa huo tangu Februari 2022.

Aidha, jumla ya watu 13,837 wamepatikana na ugonjwa huo, 338 miongoni mwao wakiwa wamelazwa hospitalini.

Kolera ni ugonjwa hatari unaosababishwa na ulaji wa chakula au unywaji wa maji yenye bakteria aina ya Vibrio cholera, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linasema.

Mtu huanza kuonyesha dalili ya ugonjwa huo kati ya saa 12 hadi siku tano baada ya kula chakula au maji yenye bakteria hizo.

Ugonjwa wa kolera umeorodheshwa kama tishio kwa afya ya umma ulimwenguni lakini unaweza kutibiwa.

Mnamo Novemba, mwaka jana, Malawi ilipokea dozi 2.9 milioni za chanjo ya kudhibiti kolera kutoka Umoja wa Mataifa (UN), huku mkurupuko wa ugonjwa huo ukienea.

Malawi ni mojawapo ya nchi masikini zaidi barani Afrika na ina jumla ya watu 18 milioni.

Wengi wao wanategemea kilimo cha mazao ya chakula kwa ajili ya matumizi nyumbani.

Hata hivyo, hali ya chakula nchini Malawi ni tete kutokana na makali ya mabadiliko ya tabia nchi.

Idadi kubwa ya visa vya maambukizi ya kolera hurekodiwa nyakati za msimu wa mvua.

Visa vya maambukizi ya kolera vimekuwa vikiripotiwa nchini Malawi tangu 1998, haswa katika maeneo ya kusini mwa taifa hilo.

Sehemu kubwa ya maeneo hayo ni tambarare na hukumbwa na mafuriko nyakati za msimu wa mvua nyingi.

Mkurupuko wa sasa wa kolera umeathiri wilaya 27 kati ya 29 nchini Malawi na kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo ndani ya miaka 10 iliyopita.

Mkurupuko huo unatokea baada ya kimbunga Ana (kilichotokea Januari 2022) na kimbunga Gombe (kilichotokea Machi 2022) kusababisha mafuriko makubwa.

Maelfu ya watu walipoteza makao kufuatia janga hilo na sasa wanakabiliwa na kero la ukosefu wa maji safi na mazingira machafu.

  • Tags

You can share this post!

Viongozi wa ODM Pwani waunga serikali ya Ruto

Kaunti zakosa kutumia pesa kwa maendeleo

T L