• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Viongozi wa ODM Pwani waunga serikali ya Ruto

Viongozi wa ODM Pwani waunga serikali ya Ruto

MAUREEN ONGALA Na WINNIE ATIENO

MUUNGANO wa Kenya Kwanza umevuna pakubwa baada ya viongozi wa chama cha ODM eneo la Pwani kukumbatia serikali ya kitaifa kwa ajili ya maendeleo ya eneo hilo.

Wakiongozwa na Gavana Abdulswamad Nassir wa Mombasa, viongozi hao wamesisitiza kuwa watashirikiana na serikali ya Rais William Ruto ili kuinua eneo hilo kiuchumi.

Wameeleza nia yao ya kufanya kazi na utawala wa nchi wakisema ni wakati wa kusonga mbele kwani kipindi cha siasa kimekwisha.

Kwa miaka mingi, eneo la Pwani limekuwa ngome ya ODM – ya Waziri Mkuu wa zamani Bw Raila Odinga – ambayo imekuwa mstari wa mbele kukosoa serikali.

Licha ya hayo kumekuwa na mabadiliko huku viongozi kama Bw Nassir na mwenzake Gavana Gideon Mung’aro wa Kilifi wakitangaza hadharani kuwa watafanya kazi na serikali kwa manufaa ya wananchi.

“Viongozi huchaguliwa na Mungu. Kuna sababu kwanini nikachaguliwa Gavana na Dkt Ruto Rais wa taifa la Kenya. Hii ni mipango ya Mungu. Ndani ya 2023 wacha tuwe watu wa kujifunza kutoka kwa historia yetu na kuungana kama jamii moja,” alisema Gavana Nassir aliyechaguliwa kupitia tikiti ya ODM mwezi Agosti.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Nassir alisisitiza kuwa kinara wake Bw Odinga ni mwanademokrasia na hana shida naye akishirikiana na serikali iliyopo mamlakani.

Spika wa Seneti Amason Kingi aliwahi kuelezea jinsi alivyokula kibaridi akiwa gavana wa Kilifi.

Kulingana naye, Kilifi ilikuwa imetengwa wala hakupata mwaliko Ikulu kukaribisha mwaka mpya sababu yake kuwa katika upinzani.

Alimshukuru Rais Ruto kwa kufanya kazi na viongozi wote licha ya kutoka vyama tofauti.

“Rais hujali kiongozi yuko upinzani au la, uko tayari kufanya nao kazi. Kama eneo tumeamua kuwa tutafanya kazi nawe, na kutembea na kuombea nchi yetu inawiri. Wewe ni kiongozi asiyebagua,” alieleza Bw Kingi.

Rais Ruto alisisitiza kuwa hatabagua kiongozi yeyote na yuko tayari kufanya kazi na wote kwa manufaa ya Wakenya.

“Tuko na viongozi walio katika serikali na wale wa upinzani, wote wanahudumia Wakenya. Wote wanapaswa kupewa heshima licha ya vyama vya kisiasa wanavyoegemea. Naomba viongozi wote wahudumie Wakenya kwa usawa,” alisema Dkt Ruto wakati wa kuvuka mwaka katika sherehe iliyoandaliwa Ikulu ya Mombasa.

Haya yakijiri, Mbunge wa Ganze, Bw Kenneth Kazungu, ameomba viongozi wa Pwani kuunga mkono serikali tawala ya Kenya Kwanza.

“Kila Mkenya hulipa ushuru kwa usawa hatupaswi kuomba huduma. Ila hapa Kenya mambo ni tofauti; walio katika serikali au wanaoiunga mkono hufaidika sana kuliko walio upinzani,” alihoji Bw Kazungu.

Alihoji kwamba muda ambao Pwani imekuwa katika upinzani imekuwa ikikosa nafasi za maendeleo.

Alisema ni wakati wa Pwani kuvuna pakubwa kwa kushirikiana na serikali kuu.

Mbunge wa Nyali, Bw Mohammed Ali, ni miongoni mwa viongozi wa Kenya Kwanza ambao wamekuwa wakiwasukuma viongozi wa Pwani walio ODM kugura chama hicho.

Hata hivyo, Mbunge wa Jomvu, Bw Badi Twalib, alisisitiza kuwa hawatamtoroka Bw Odinga.

  • Tags

You can share this post!

Atwoli aunga mkono hatua ya Sakaja kuondoa matatu CBD...

Kolera: Ufunguzi wa shule waahirishwa Malawi

T L