• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Mabadiliko ya tabianchi yaweka Afrika katika hatari ya janga la malaria, kipindupindu

Mabadiliko ya tabianchi yaweka Afrika katika hatari ya janga la malaria, kipindupindu

NA PAULINE ONGAJI

[email protected]

KIGALI, RWANDA

BARA la Afrika linakumbwa na hatari ya kukabiliwa na janga la maradhi ya malaria na kipindupindu kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Haya ni kulingana na wataalam wa kiafya wanaohudhuria Kongamano la Kimataifa kuhusu ajenda ya afya barani Afrika (AHAIC 2023), linaloendelea jijini Kigali, Rwanda.

Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa kongamano hilo, Dkt Ahmed Ogwell Ouma, Kaimu Mkurugenzi wa Africa CDC, alisema kwamba mabadiliko ya tabianchi yameendelea kusababisha athari za kiafya barani.

“Majanga kama vile mafuriko na ukame miongoni mwa mengine, yameathiri mifumo ya afya kwa sababu majanga haya huathiri huduma za afya na hivyo kuchangia maradhi haya,” akasema Dkt Ahmed Ogwell.

Kulingana na Dkt Gitahi Githinji, Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika la Amref Health Africa, uhaba wa maji kutokana na ukame, vile vile mafuriko, vimeathiri mifumo ya maji katika sehemu mbali mbali za bara hili, na hivyo kuchangia kuongezeka kwa visa vya kipindupindu.

Kwa sasa Afrika inakumbwa na mabadiliko makali ya tabianchi huku eneo la upembe wa Afrika likikumbwa na ukame mbaya zaidi kuwahi shuhudiwa katika kipindi cha miongo minne.

Mojawapo ya mataifa yaliyoathirika pakubwa na kipindupindu ni Malawi, ambapo taifa hili la  kusini mwa Afrika limerekodi zaidi ya visa 40,000 vya kipindupindu na takriban vifo 1,500 tangu mwanzo wa mkurupuko wa maradhi hayo mwezi March 2022.

“Huku mkurupuko wa maradhi mengi ukirekodiwa kwa kawaida katika msimu wa mvua, mwaka jana mardhi haya yalianza katika msimu wa kiangazi. Mvua ilipoanza kunyesha nayo ikazidisha msambao wa maradhi yanayotokana na maji,” asema Dkt Alinafe Kasiya, Mkurugenzi wa shirika la VillageReach nchini Malawi. Shirika hili hutoa suluhu za kiafya katika jamii za mapato ya chini.

Nchini Kenya, kufikia Januari 2023, Shirikisho la kimataifa la shirika la Msalaba Mwekundu IFRC lilikuwa imethibitisha visa vya kipindupindu katika kaunti 12 nchini. Kwa upande mwingine, kuna zaidi ya visa milioni 3.5 vya malaria nchini, huku zaidi ya vifo 10,700 kutokana na maradhi haya vikisajiliwa kila mwaka. Duniani, Shirika la Afya Duniani WHO linakadiria kwamba zaidi ya watu 400,000 ulimwenguni, hufa kutokana na maradhi haya.

Kulingana na Dkt Githinji, mabadiliko ya tabianchi ni tishio kwa mifumo ya afya kwani pia yamehusishwa na maradhi yasiyosambaa kama vile magonjwa ya moyo, majeraha na vifo vya mapema.

Ili kuangazia suala hili, Dkt Adelheid Onyango, Mkurugenzi wa Mfumo wa afya kwa wote katika Shirika la Afya Duniani hapa barani, serikali za Afrika sharti ziwekeze mikakati ya kutoa onyo mapema za majanga yanayosababishwa na tabianchi.

“Ili kufanikiwa, serikali za Afrika zinapaswa kushirikiana kwa karibu na jamii ili kubuni suluhu thabiti.”

Rwanda tayari imechukua hatua moja ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Miaka saba iliyopita, nchi hiyo ilizindua Kigali Car Free Day, siku rasmi ambapo watu hawaruhusiwi kutumia usafiri wa magari. Siku hii huadhimishwa kila Jumapili ya kwanza na ya tatu kila mwezi, kama mbinu ya kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuthibitisha hatua za kukabiliana na maradhi yasiyosambaa (NCDs).

  • Tags

You can share this post!

Wenyeji wadaiwa kula uroda kwa uwanja wa michezo

Yafichuka mtunzi Enock Ondego alifariki baada ya serikali...

T L