• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Maradhi ya wanyama hadi kwa binadamu kuzidi – UN

Maradhi ya wanyama hadi kwa binadamu kuzidi – UN

NA AFP

GENEVA, USWISI

WATAALAMU wameonya kuwa huenda maradhi yanayotoka kwa wanyama hadi kwa binadamu yakaibua janga jingine hatari la maradhi ya kuambukizana kote duniani.

Hii ni baada ya maradhi ya homa ya nyani kuibuka miezi michache tu kabla ya mataifa mengi duniani kufanikiwa kukabili kikamilifu janga la virusi vya corona.

Ijapokuwa homa ya nyani imekuwepo kwa muda mrefu, wataalamu wanasema mchipuko wake umeongezeka sana katika siku za hivi karibuni.

Wanasema hali hiyo imechangiwa sana na ukataji miti, mabadiliko ya hali ya hewa kati ya masuala mengine yanayolingana na mahusiano kati ya binadamu na wanyama.

Maradhi mengine yaliyotoka kwa wanyama hadi binadamu ni virusi vya HIV, Ebola, Zika, SARS, MERS, homa ya ndege na tauni.Jumamosi, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema kuwa bado linaendelea kuchunguza chimbuko la virusi vya corona.

Hata hivyo, wataalamu wanasema ushahidi mkubwa uliopo unaonyesha kuwa virusi hivyo vilitoka kwa wanyama.

Huku visa vya homa ya nyani vikifikia karibu 1,000 kote duniani, WHO imeonya kuwa kuna hatari kubwa maradhi hayo “yakageuka janga hatari” katika nchi nyingi duniani.Wiki iliyopita, Mkurugenzi wa Mikasa katika shirika hilo, Michael Ryan, alisema kuwa mbali na homa ya nyani, kuna “hatari majanga zaidi yakazuka kutokana na mwingiliano kati ya binadamu na wanyama.”

“Kasi ya jinsi maradhi haya yanatoka kwa wanyama hadi kwa wanadamu inaongezeka sana,” akaeleza.

Homa ya nyani haikuibuka juzi, bali kisa cha kwanza kilibainika nchini DRC Congo mnamo 1970.

Kufikia sasa, chimbuko la maradhi hayo linadaiwa kuwa Afrika ya Kati na Magharibi.

“Licha ya jina lake, chimbuko la homa hiyo halina uhusiano wowote na nyani,” akasema Olivier Restif, ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya kuambukizana katika Chuo Kikuu cha Cambridge.

Alisema licha ya baadhi ya chimbuko la maradhi hayo kuwa wanyama, wanadamu ndiyo huwa wanayasambaza sana.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kusimamia Mazingira (UNEP), asilimia 60 ya maradhi ya wanadamu yanatoka kwa wanyama.

Shirika hilo pia lilisema kuwa asilimia 75 ya maradhi ya kuambukizana yanayoibuka kwa sasa miongoni mwa wanadamu yanatoka kwa wanyama.

“Maradhi hayo yamechangiwa na ongezeko la binadamu, ongezeko la wanyama na kuingiliwa kwa makazi asilia ya wanadamu.”

Akaongeza: “Wanyama wa pori wamebadilisha mienendo yao sana kutokana na shughuli za kilimo zinazoendeshwa na wanadamu. Wengi wameanza kutoka katika makazi yao asilia na kutafuta mengine.”

Kulingana na Benjamin Roche, ambaye ni mtaalamu wa magonjwa katika Taasisi ya Utafiti na Maendeleo ya Ufaransa (FIRD), ukataji miti umechangia sana ongezeko la maradhi hayo.

“Ukataji miti huathiri sana mazingira. Tunawapoteza wanyama ambao kwa hudhibiti msambao wa virusi. Ni hali pia inayotoa nafasi kwa virusi hivyo kusambaa virahisi ba haraka,” akasema.

Wataalamu wanasema kuna uwezekano hali hiyo kuongezeka, baada ya utafiti uliotolewa majuzi kuonyesha huenda mabadiliko ya hali ya hewa yakachangia kuibuka kwa janga jingine.

  • Tags

You can share this post!

Ruto na Raila wapigania miradi ya Rais

EACC yamulika Kilifi kuhusu Sh1.1 bilioni za mawakili

T L