• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 12:03 PM
Ruto na Raila wapigania miradi ya Rais

Ruto na Raila wapigania miradi ya Rais

NA WAANDISHI WETU

MIRADI iliyoanzishwa na Serikali ya Jubilee inayokadiriwa kugharimu takriban Sh1.4 trilioni katika ukanda wa Pwani, inazidi kugeuzwa chambo kwa kampeni za wawaniaji urais kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Agosti.

Kiongozi wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga, anayewania urais kwa chama cha Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, na mpinzani wake mkuu, Naibu Rais William Ruto, wa chama cha UDA kilicho ndani ya Kenya Kwanza, wote wamekuwa wakitumia miradi hiyo kama kivutio kwa wapigakura.

Dkt Ruto, anapozuru kaunti za Pwani, hutaja miradi hiyo kama baadhi ya dhihirisho kuwa ana uwezo wa kuleta mafanikio zaidi endapo atashinda urais ikizingatiwa yeye ndiye naibu rais katika Serikali ya Jubilee.

Kwa upande wake, Bw Odinga husifu baadhi ya miradi hiyo akisema kuna mingine ambayo ilikuwa imewekewa msingi alipokuwa waziri mkuu chini ya uongozi wa aliyekuwa rais marehemu Mwai Kibaki.

Katika manifesto ya Azimio iliyozinduliwa wiki iliyopita, mahitaji ya kukamilisha miradi kama vile upanuzi wa bandari za Mombasa na Lamu, kuanzisha maeneo ya kiviwanda, na kuendeleza miradi ya kustawisha uvuvi yalitiliwa mkazo.

Rais Uhuru Kenyatta hudai kuwa, utekelezaji wa miradi Pwani umefanikishwa katika awamu ya pili ya uongozi wake kwa sababu ya ushirikiano ulioletwa na handisheki iliyotuliza nchi kisiasa.

“Wananchi lazima mjiulize mwatakaje. Mwataka umoja, utulivu na maendeleo kama haya ambayo yatatusaidia kuletea wananchi maisha mazuri ama mwataka porojo ambayo haimalizi umaskini. Shauri yenu, kila mtu ana haki ya kufanya vile anataka lakini mjiulize ni ‘barabara’ gani mnayotaka kupitia,” Rais alisema, alipozuru Mombasa mapema mwaka 2022.

Rais husisitiza kuhusu hitaji la kuwepo uongozi ambao utaiendeleza nchi mbele wakati atakapostaafu urais baada ya uchaguzi wa Agosti 9.

Baadhi ya miradi ambayo serikali inajitahidi kukamilisha ni ujenzi wa barabara ya Dongo Kundu Southern Bypass katika Kaunti ya Mombasa, upanuzi wa barabara ya Mombasa-Mtwapa, ujenzi wa bwawa la Mwache, upanuzi wa lile la Mzima 2 miongoni mwa mabwawa mengine inayokusudiwa kusuluhisha tatizo la maji safi Pwani.

Mradi mwingine ni ukarabati wa bandari ya samaki ya Shimoni, Kaunti ya Kwale ambayo inakumbwa na pingamizi mahakamani kuhusu utoaji wa zabuni.

Miongoni mwa miradi iliyokamilika japo kwa awamu ni ujenzi wa kituo cha pili cha meli katika bandari ya Mombasa, awamu ya kwanza ya bandari ya Lamu, kituo kipya kikuu cha mafuta cha Kipevu, ufufuzi wa shirika la kiserikali la meli (KNSL) na miradi mingi ya ujenzi wa barabara ikiwemo daraja la Makupa.

Serikali imesisitiza kuwa, hakuna mradi wowote kati ya ile iliyoanzishwa utakaoachwa katikati na kugeuka ‘mradi hewa’ katika miaka ya usoni.

“Kwa miradi ambayo imekamilika, tunasubiri tu rais azindue rasmi,” afisa anayehusika katika mipango ya utekelezaji miradi ya serikali, aliambia Taifa Leo.

Mnamo Januari, Kamati ya Kiufundi ya Utekelezaji wa Maendeleo Kitaifa (NDITC) ikiongozwa na mwenyekiti wake, Dkt Karanja Kibicho, ilihakikishia Wakenya kwamba miradi yote itakamilika kwa wakati ufaao.

Ripoti za Winnie Atieno, Kennedy Kimanthi na Valentine Obara

  • Tags

You can share this post!

WANTO WARUI: Wamiliki shule za kibinafsi wadai kuhangaishwa...

Maradhi ya wanyama hadi kwa binadamu kuzidi – UN

T L