• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 2:59 PM
Mwanawe Museveni atangaza azma yake kuwa rais wa Uganda

Mwanawe Museveni atangaza azma yake kuwa rais wa Uganda

NA AFP

KAMPALA, Uganda

MWANAWE Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, kwa mara ya kwanza ametangaza azma yake ya kuongoza taifa hilo.

Kwa muda mrefu, wanachanganuzi wamekuwa wakibashiri Muhoozi Kianerugaba amekuwa akiandaliwa kwa wadhifa huo mkubwa nchi.Ni juzi tu ambapo Muhoozi aliibua mtafaruku wa kidiplomasia na Kenya kwa kutisha kuvamia Nairobi.

“Zawadi ambayo ninaweza kumpa mamangu mpendwa ni kuwa Rais wa Uganda! Bila shaka nitafanya hivyo!” Jenerali Muhoozi, 48, akasema katika mtandao wa kijamii wa Twitter.

Ingawa, siku za nyuma Muhoozi amekana madai kwamba analenga kumrithi babake Museveni, mwenye umri wa miaka 78, amepandishwa cheo haraka katika jeshi la Uganda.

Hatua hiyo imeendeleza uvumi nchini humo na ukanda wa Afrika Mashariki kwamba anaandaliwa kumrithi babake, ambaye ni mmoja wa marais wa Afrika ambao wamehudumu mamlakani kwa muda mrefu zaidi.

Museveni ameshikilia wadhifa huo kwa miaka 36, tangu 1986.

Baada Muhoozi kushutumiwa na wengine kutokana na jumbe zake mtandaoni, Rais Museveni alimshauri akome kutumia Twitter kujadili masuala mazito ya nchi.

Badala yake alimtaka aitumie kupitishia kauli zake kuhusu michezo na burudani. Lakini mwana huyo ameonekana kumkaidi babake kwa kuendelea kutupa jumbe zenye mada nzitonzito.

Wiki jana aliandikia: “Mimi ni mtu mzima na hakuna anayeweza kunipiga marufuku kitu au suala lolote!”

Awali, Rais Museveni alikuwa ameomba msamaha kwa taifa jirani la Kenya baada ya mwanawe huyo, miongoni mwa kauli zingine, kutisha kupeleka wanajeshi wakateke jiji kuu la Nairobi.

Kauli hiyo iliwakera Wakenya waliomshambulia Muhoozi kwenye Twitter.

Walimtaka Rais Museveni adhibiti mwanawe wakisema kauli hizo zinaweza kuvuruga uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili, kando na kuibua uhasama miongoni mwa raia wao.Hata hivyo, Museveni alimtetea kinana wake akimtaja kama “jenerali mzuri”.

Baada ya hapo alimpokonya wadhifa wa kamanda wa jeshi la nchi kavu la Uganda, ila akampandisha cheo hadi kuwa jenerali.

Kwa mtazamo wa wengi Uganda, dalili za Muhoozi kuwa mrithi wa urais zilianza kuonekana kitambo alipokwezwa vyeo haraka jeshini.

Lakini awali serikali imechukua msimamo mkali kuhusu suala hilo, ikipinga kujadiliwa kwake na mtu yeyote.

Mnamo 2013, polisi walizima kuchapishwa kwa magazeti mawili ya kibinafsi na matangazo katika vituo viwili vya redio kwa siku 10.

Hii ni baada ya vyombo hivyo vya habari kutangaza hadharani taarifa ya kisiri iliyotolewa na mwanajeshi mmoja wa cheo cha juu, ikidai Rais Museveni anamwandaa Kianerugaba kuwa mrithi wake.

Kauli za Kianerugaba kuhusu masuala nyeti ya sera za kigeni, mara nyingi, zimesababisha utata katika serikali ya Uganda na mahusiano yake na mataifa ya kigeni.

Kwa mfano, kauli zake za kuunga mkono waasi wa Tigray ilikera Serikali ya Ethiopia. Kauli zake kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na mapinduzi ya mwaka 2021 nchini Guinea pia ziliibua maswali mengi.

  • Tags

You can share this post!

Omanyala, Kipchoge wasuka dili ya kukuza talanta

Mamilioni ya UDA na ODM kila mwezi

T L