• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 11:39 AM
Putin aombwa aketi na Zelensky wamalize vita

Putin aombwa aketi na Zelensky wamalize vita

NA MASHIRIKA

BERLIN, UJERUMANI

UFARANSA na Ujerumani zimemrai Rais Vladimir Putin wa Urusi kufanya mazungumzo ya kina na ya moja kwa moja na mwenzake wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, kama njia moja ya kumaliza mzozo kati ya nchi hizo mbili.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani walisema hiyo ndiyo njia pekee ambapo mzozo huo utapata suluhisho la kudumu.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na serikali ya Ujerumani, Scholz na Macron walizungumza na Putin kwa zaidi ya dakika 80 kwa njia ya simu.

“Viongozi hao wawili walimrai Putin kusitisha mashambulio yake dhidi ya Ukraine na kuondoa majeshi yake nchini humo mara moja,” ikasema Ujerumani.

Kwa upande wake, Putin alisema kuwa Urusi iko tayari kurejelea mazungumzo kati yake na Ukraine kama ilivyokuwa hapo awali.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikueleza uwezekano wa Putin kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Zelenzky.

Awali, Zelensky alisema hakuwa tayari kufanya mazungumzo na Putin, japo akaeleza kuhusu haja ya kumaliza mapigano hayo.

Wajumbe tofauti kutoka nchi hizo mbili wamekuwa wakifanya mazungumzo kumaliza mzozo huo bila mafanikio tangu Februari vita kati ya nchi hizo vilipoanza.

Mataifa hayo mawili pia yalimrai Putin kuwaachilia wapiganaji 2,500 wa Ukraine iliowakamata katika kituo cha kutengeneza vyuma cha Azovstal, jijini Mauripol.

Urusi ilifanya msururu wa mashambulio makali katika kiwanda hicho kwenye juhudi za kukitwaa kutoka kwa vikosi vya Ukraine.

Mapema mwezi huu Mei, maafisa wa serikali ya Urusi walisema wapiganaji waliokuwa wakikilinda kiwanda hicho dhidi ya kutekwa na majeshi yake walijisalimisha kwake bila masharti yoyote.

Hata hivyo, Zelensky anasisitiza Urusi iliwashinikiza kujisalimisha kwake la sivyo iwaue.

Urusi imesema hapo awali kuwa zaidi ya wapiganaji 900 kutoka kituo hicho walipelekwa kwenye gereza jipya katika kijiji cha Olenivka, kilicho katika eneo la Donetsk, inaloshikilia hadi sasa.

Ukraine imekuwa ikisema inatarajia Urusi itawaachilia wapiganaji hao kama sehemu ya makubaliano ya kumaliza mzozo huo, ijapokuwa Urusi haijatoa thibitisho lolote.

Baadhi ya wabunge wa Urusi wanashikilia kuwa wapiganaji hao wanapaswa kunyongwa au kuuawa kwa kupigwa risasi.

Vile vile, wakati wa mazungumzo hayo, viongozi hao wawili walimrai Putin kuwaondoa wanajeshi wake katika mji wa bandari wa Odesa nchini Ukraine, ili kuiruhusu nchi hiyo kusafirisha au kupokea bidhaa kutoka mataifa ya nje.

Kwa upande wake, Urusi pia ilizionya Ujerumani na Ufaransa dhidi ya kupeleka silaha zaidi nchini Ukraine, zikisema kuwa huenda hilo likazidisha mzozo huo.

 

  • Tags

You can share this post!

Ugatuzi: Kilio cha magavana

Polisi wafuatilia madai dhidi ya mbunge wa Bahati

T L