• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Ugatuzi: Kilio cha magavana

Ugatuzi: Kilio cha magavana

NA SHABAN MAKOKHA

MAGAVANA wanaoondoka wametaja ukosefu wa nia njema ya kisiasa kuwa kizingiti katika utekelezaji wa mfumo wa ugatuzi katika kaunti zote nchini.

Hali hii, magavana hao wanasema, ni licha ya kwamba mfumo huo wa utawala ulikuwa ni wazo zuri kwa sababu unatarajiwa kuwawezesha wananchi kupata huduma muhimu karibu nao.

Kando na huduma, ugatuzi pia unalenga kufanikisha maendeleo, na miradi mingine ya kiuchumi, katika ngazi za mashinani.

Lakini Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya, amesema tofauti za mara kwa mara kati ya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti kuhusu ufadhili wa majukumu ya kaunti, ukosefu wa mashauriano kuhusiana na masuala yanayoathiri kaunti, Wizara ya Fedha kuchelewa kutuma fedha kwa serikali za kaunti ni miongoni mwa changamoto zilizoathiri utekelezaji wa ugatuzi tangu 2013.

“Nia njema ya kisiasa ndiyo hitaji muhimu la kufanikisha utekelezaji wa ugatuzi. Kwa kufeli kutoa fedha za kutosha kwa kaunti, viongozi wa kitaifa wanaangamiza ugatuzi ambao unalenga kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo mashinani. Ikiwa Rais hataunga mkono ugatuzi, ndoto hiyo haitatimia,” Bw Oparanya akaeleza.

“Aidha, juhudi za kuimarisha maisha ya wananchi katika ngazi za mashinani hazitafikiwa,”akaongeza gavana huyo anayehudumu muhula wake wa pili na wa mwisho.

Ushirikishaji umma Bw Oparanya aliwataka watekelezaji wa ugatuzi kushirikisha umma katika mipango yao, kukumbatia usawa wa kijinsia na kuwapa raia mamlaka ya kusimamia miradi.

Hata hivyo, alisema licha ya changamoto zinazokumba utekelezaji wa mfumo huo nchini, ugatuzi umechochea maendeleo haswa katika maeneo ya mashambani kote.

“Nawahimiza walioko mamlakani kuhakikisha kuwa maamuzi yote wanayofanya wanajali maslahi ya wananchi. Wananchi washirikishwe katika maamuzi muhimu,” Bw Oparanya, ambaye amewahi kuwa mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG), akasema.

Kwa upande wake Gavana wa Busia, Bw Sospeter Ojaamong, alisema kuwa ili ugatuzi ufaulu, utahitaji kuwa na mazingira ya kuhusishwa kwa wadau wote katika mchakato wa utekelezaji.

“Ili kufanikisha ugatuzi, sharti kuwe na uhusiano mzuri katika ya ngazi zote mbili za utawala. Bunge, serikali za kaunti, Wizara na Afisi Huru na Tume mbalimbali za Kikatiba zinafaa kufanya kazi pamoja,” akasema Bw Ojaamong.

Gavana huyo alizitaka asasi za serikali za kaunti kukumbatia teknolojia mpya, mbinu za kisasa za usimamizi, sera na uzingatiaji wa utawala wa kisheria ili kudumisha mfumo huo.

“Ugatuzi ulionekana kama njia kuu ya kupiga jeki maendeleo na kusambaza majukumu. Unawezesha serikali za kaunti kutambua shida, kuunda sera, kupanga na kukusanya mapato na kutekeleza bajeti zao. Lakini kucheleweshwa kwa mgao wa fedha kutoka Hazina ya Kitaifa kumezuia kufikiwa kwa malengo haya,” Bw Ojaamong akaongeza.

  • Tags

You can share this post!

Karan Patel ndiye mfalme wa Eldoret Rally

Putin aombwa aketi na Zelensky wamalize vita

T L