• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 11:54 PM
Rais wa zamani Tunisia asukumwa jela miaka 4

Rais wa zamani Tunisia asukumwa jela miaka 4

TUNIS, Tunisia

Na MASHIRIKA

MAHAKAMA moja nchini Tunisia imemhukumu aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Moncef Marzouki, miaka minne gerezani kwa shtaka la “kuhatarisha” usalama wa taifa hilo, vilisema vyombo vya habari jana.

Kiongozi huyo wa zamani hakuwepo wakati hukumu hiyo ilipotolewa dhidi yake.Marzouki, 76, amekuwa akiishi uhamishoni nchini Ufaransa kwa miaka mitatu iliyopita.Awali, alikuwa ameitisha maandamano makubwa dhidi ya utawala wa Rais Kais Saided. Kulingana na vyombo vya habari nchini humo, Marzouki alipatikana na hatia ya “kutishia uthabiti wa usalama wa taifa hilo kutoka ughaibuni anakokaa.

”Vile vile, alipatikana na hatia ya “kuvuruga uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tunisia na Ufaransa.”Hata hivyo, kiongozi huyo alipinga vikali uamuzi huo, akisema “ulitolewa na rais ambaye hakuchaguliwa kidemokrasia na anayeendelea kuivunja katiba.”Alisema mashtaka dhidi yake ni “ukiukaji wa haki na ukweli.”

Alieleza kuwa badala yake, Saided ndiye anayepaswa kushtakiwa kwa “kujipa mamlaka asiyostahili” mnamo Julai.“Nimejitolea kuendelea kukabiliana na udikteta katika nchi yangu hadi nitakapofariki. Sitamwambia wakili yeyote kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo,” akasema.

Hata hivyo, wakili wake, Lamia Khemiri, aliwaambia wanahabari kwamba Marzouki hajapewa maagizo yoyote kufika mahakamani, hivyo hajui sababu ambapo alihukumiwa.Saied alichaguliwa kuwa rais mnamo Julai 2019. Mnamo Julai 25, mwaka huu, aliivunja serikali yake, Bunge na kuanza harakati kali kukabiliana na ufisadi.Hilo ni baada ya taifa hilo kukumbwa na mizozo ya kiuchumi na kisiasa kwa miezi kadhaa.

Mnamo Septemba, alijiongezea mamlaka zaidi, akiapa kutozingatia Katiba kwa namna yoyote ile.Badala yake, alisema ataliongoza taifa hilo kwa kutoa amri na maagizo anayoona yatakuwa ya manufaa kwa mustakabali wake. Licha ya hilo, aliahidi kuandaa mazungumzo kuangazia na kutathmini mabadiliko hayo.

Mapema mwezi huu, alitangaza bunge litabaki limevunjwa hadi Desemba 17 mwaka ujao, ambapo uchaguzi mpya utafanyika.Mbali na hayo, alitangaza majuma 11 ya “mashauri ya kina” ili “kubuni rasimu mpya ya katiba na mageuzi mengine muhimu ya kiutawala” kabla ya nchi hiyo kuandaa referenda Julai 25, 2022 kuiwezesha kupata katiba mpya.

Marzouki ametaja hatua za Saied kama mapinduzi ya kiutawala, huku akiwaomba raia kufanya maandamano makubwa dhidi yake.Vile vile, amezirai nchi zilizotawaliwa na Ufaransa kuhamisha mkutano wao wa kimataifa unaoendelea jijini Tunis.Licha ya kuwa uhamishoni, kiongozi huyo amekuwa akitumia vyombo vya habari kama televisheni kuendeleza ukosoaji dhidi ya Saided, anayemtaja kuwa “dikteta.”

Kwenye maandamano yaliyofanyika jijini Paris mnamo Oktoba, Marzouki aliirai serikali ya Ufaransa “kusimamisha usaidizi wowote ambao imekuwa ikitoa kwa utawala wa Saied.”Kwa upande wake, Saied amekanusha madai ya kuipindua serikali na kutozingatia Katiba.Badala yake, amemtaja Marzouki kuwa “adui mkubwa” wa Tunisia.

Ameziomba mahakama kuchunguza taarifa ambazo Marzouki amekuwa akitoa na kufutilia mbali paspoti yake.Baadhi ya mataifa ya Magharibi yamemrai Saied kurejesha uzingatiaji wa kikatiba, demokrasia na uhuru wa watu kujieleza kama njia ya kujenga imani yazo dhidi ya utawala wake.

Baada ya maasi ya kiutawala yaliyoikumba Tunisia mnamo 2011, Bunge lilimchagua Marzouki kuwa rais wa mpito.Alilisaidia taifa hilo kupata katiba mpya mnamo 2014.Hii si mara ya kwanza kwa Marzouki kufikishwa mahakamani au kushtakiwa. Kabla ya kuchaguliwa kuwa rais wa mpito na Bunge, alikuwa ameshtkakiwa karibu mara saba.

You can share this post!

Mchezaji wa zamani wa Gor atua Somali

JUMA NAMLOLA: Krismasi iwe mwalimu kuhusu kuwajali wengine...

T L