• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Shambulio la kigaidi jijini laua 9 na kujeruhi wengi

Shambulio la kigaidi jijini laua 9 na kujeruhi wengi

MOGADISHU, SOMALIA

TAKRIBAN watu tisa wameaga dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa kwenye mashambulizi mawili ya mabomu yaliyotokea wakati mmoja Somalia.

Maafisa wa usalama walithibitisha matukio hayo wakisema bomu lilitegwa ndani ya gari katika mji wa katikati mwa Somalia Jumatano.

“Magaidi walishambulia mji wa Mahas asubuhi kwa kuweka mabomu kwenye magari,” akasema afisa wa usalama wa eneo hilo Abdullahi Adan.

“Magaidi hao walikuwa wakilenga eneo la raia na tumethibitisha kuwa watu tisa, wote wakiwa raia, walikufa katika milipuko hiyo miwili,” akaongeza Adan.

Shambulio hilo linalohusishwa na wapiganaji wa jihadi wa Al-Shabaab, lilifanyika katika eneo la Hiran katikati mwa Somalia, ambapo mashambulizi makubwa yalifanywa mwaka jana dhidi ya kundi hilo lenye uhusiano na Al-Qaeda.

“Magaidi, baada ya (kushindwa) waliamua kuwalenga raia, lakini hii haitazuia nia ya serikali kuendelea kupambana nao,” akasema Osman Nur, kamanda wa polisi huko Mahas.

“Wameua raia wasio na hatia katika milipuko.”

Walioshuhudia walisema milipuko hiyo ilitokea karibu na mkahawa mmoja karibu na jengo la utawala la wilaya huko Mahas.

“Walioangamia kwenye shambulio hilo ni wanawake, watoto na wanaume. Ni watu ambao hawana hatia,” akasema Adan Hassan, aliyeshuhudia tukio hilo.

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alitangaza vita vikali dhidi ya wapiganaji wa Al-Shabaab, ambao wamekuwa wakiwahangaisha wananchi.

Mnamo Julai 2022, wanamgambo wa kiukoo wanaojulikana kama Macawisley walianzisha uasi dhidi ya Al-Shabaab katika sehemu za katikati mwa Somalia, na Rais Mohamud alituma wanajeshi Septemba kusaidia kupambana na kundi hilo.

Katika miezi ya hivi karibuni, wanajeshi wametwaa tena maeneo mengi katika majimbo ya kati ya Galmudug na Hirshabelle katika operesheni iliyoungwa mkono na mashambulio ya anga ya Amerika na kikosi cha Umoja wa Afrika (AU) kinachojulikana kama ATMIS.

Hata hivyo, waasi hao mara kwa mara wamelipiza kisasi kwa kutekeleza mashambulizi mbalimbali wakisisitiza uwezo wao wa kushambulia katikati mwa miji ya Somalia na vituo vya kijeshi.

Japo walilazimishwa kutoroka katika vituo vikuu vya mijini takriban miaka 10 iliyopita, Al-Shabaab bado wamejikita katika maeneo makubwa ya vijijini katikati na kusini mwa Somalia huku wakitekeleza mashambulizi kila mara na kuwaua wengi.

Mnamo Oktoba 29, watu 121 katika mji mkuu wa Mogadishu waliuawa katika milipuko miwili ya bomu lililotegwa kwenye gari katika eneo la wizara ya elimu.

  • Tags

You can share this post!

MAPISHI KIKWETU: Jinsi ya kuandaa shakshuka

Washukiwa watatu wa ugaidi kusota seli kwa wiki moja zaidi

T L