• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 5:50 AM
Washukiwa watatu wa ugaidi kusota seli kwa wiki moja zaidi

Washukiwa watatu wa ugaidi kusota seli kwa wiki moja zaidi

NA BRIAN OCHARO

MAHAKAMA ya mjini Mombasa imewaruhusu polisi waendelee kuwazuilia washukiwa watatu wanaodaiwa kula njama ya kushambulia kigaidi eneo la burudani mjini Diani, Kwale.

Musab Abdulnasir Kassim na Mistwah Abdulnasir Kassim walikamatwa kuhusiana na ripoti kuwa walikuwa wakielekea Kwale kujiunga na washirika wao ili kutekeleza shambulio la kigaidi mkesha wa Mwaka Mpya 2023.

Inadaiwa walipatikana wakiwa na bastola aina ya Glock ya Austria ikiwa na risasi 15.

Baadaye polisi pia walimkamata Aisha Abdalla Musa eneo la Kizingo, Mombasa, Januari 1, mwendo wa saa kumi na moja jioni.

Watatu hao sasa wako kizuizini wakisaidia polisi katika uchunguzi.

Kulingana na hati ya kiapo ya afisa wa Kitengo cha Polisi cha Kupambana na Ugaidi, Japheth Yagan, Musab na Mistwah walikuwa wakielekea Diani kukutana na magaidi wawili wasiojulikana walipokamatwa mnamo Desemba 31 mwendo wa saa tatu usiku katika kivuko cha Likoni Bara.

“Kulikuwa na habari za kijasusi kuhusu shambulio karibu na jumba maarufu la burudani eneo la Diani wakati wa sherehe za kuvuka mwaka,” Bw Yagan alisema katika kiapo.

Huku akiomba mahakama kumpa muda zaidi wa kuwazuilia watatu hao, Bw Yagan alidai, kupitia kwa kiongozi wa mashtaka Yassir Mohamed, kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa washukiwa hao pia wanahusishwa na msururu wa wizi katika kisiwa cha Mombasa.

“Kuna taarifa za kijasusi kuwa kuna washukiwa wanaojifanya waendeshaji pikipiki katika mji wa Mombasa wenye nia ya kuendeleza ugaidi,” mwendesha mashtaka alimweleza Hakimu Mkuu Mkazi wa Mombasa Ritah Orora.

Mahakama pia iliambiwa kwamba simu za mkononi zilizopatikana kwa washukiwa zimetumwa kwa Maabara ya Uchunguzi wa kimatandao kwa uchunguzi zaidi.

Bunduki na risasi hizo pia zimetumwa kwa makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) jijini Nairobi kwa uchunguzi zaidi.

“Muda ambao umepita tangu wahojiwa wakamatwe hautoshi kufanya uamuzi wowote, kwa hivyo, ninaomba muda wa kukamilisha upelelezi kabla ya kufikia uamuzi wa kuwashtaki au la,” alisema.

Huku akiwaombea wapelelezi siku 15 kuwazuilia washukiwa hao, Bw Mohamed aliiambia korti kuwa watuhumiwa hao pia walishikwa na aina ya dawa ambayo polisi wanadai kuwa ni ya kulveya.

“Ninachunguza kesi kuhusu mwanachama wa kikundi cha kigaidi, njama ya kufanya kitendo cha kigaidi na kumiliki bunduki bila cheti. Bado hatujaandikisha taarifa ya mashahidi wengine wakuu na kuwatia mbaroni washukiwa zaidi,” akasema Bw Yagan.

Bw Mohamed aliambia mahakama kwamba madai dhidi ya washukiwa hao ni mazito sana, kwa hivyo, wapelelezi wanahitaji muda wa kutosha kufahamu uhalifu ambao washukiwa walikuwa karibu kutekeleza walipokamatwa.

Hata hivyo, washukiwa hao walipinga ombi hilo na kuieleza mahakama kuwa polisi wamekuwa na muda wa kutosha kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo.

Kupitia kwa wakili wao, walisisitiza kuwa hawana hatia huku wakipuuza madai ya wapelelezi dhidi yao.

Hakimu huyo, hata hivyo, aliwaruhusu polisi kuwashikilia kwa wiki moja tu.

Kesi hiyo itatajwa Januari 10.

  • Tags

You can share this post!

Shambulio la kigaidi jijini laua 9 na kujeruhi wengi

Mwinyi apiga tizi balaa akilenga kuitwa Hit Squad

T L