• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 8:00 AM
Tetemeko kubwa lapiga Haiti na kuua watu 1,200

Tetemeko kubwa lapiga Haiti na kuua watu 1,200

Na MASHIRIKA

WATU zaidi ya 1,200 wamefariki kufikia Jumatatu asubuhi na wengine 1,800 kujeruhiwa baada ya tetemeko kubwa la ardhi kutokea kusini magharibi mwa Haiti, maafisa wa serikali wamesema.

Tetemeko hilo liliporomosha makanisa, hoteli, shule na nyumba za makazi.Ni janga la hivi punde kukumba nchi hiyo maskini katika visiwa vya Caribbean.

Kituo cha kufuatilia mitetemeko ya ardhi cha Amerika (USGS), kilisema tetemeko hilo lilikuwa la kipimo cha 7.2 kwenye richa na lilitokea kilomita nane kutoka mji wa Petit Trou de Nippes – ulio umbali wa kilomita 150 magharibi mwa jiji kuu Port-au-Prince.

Hii ilifanya tetemeko hilo kuwa mbaya zaidi kuliko lililoua maelfu ya watu katika taifa hilo la kisiwani miaka 11 iliyopita.

Tukienda mitamboni jana, taarifa zilisema idadi ya waliofariki ilikuwa imefika 700 huku maelfu wakikosa kupatikana baada ya mkasa huo.Juhudi za kwanza za uokoaji zilizotekelezwa na raia zilisaidia kunusuru watu wengine wengi.

Ripoti pia zilisema nyumba 949, makanisa saba, hoteli mbili na shule tatu ziliharibiwa kabisa wakati wa tetemeko hilo

.Nyumba zingine 723, gereza moja, vituo vitatu vya afya na shule saba ziliathiriwa ingawa hakukuwa na uharibifu katika bandari, uwanja wa ndege na miundo msingi ya mawasiliano.

Kituo cha USGS kilisema kwamba mnamo Jumamosi tetemeko jingine la kipimo cha 5.8 kwenye richa, linalohusishwa na la kwanza, lilikumba eneo hilo.

Athari za tetemeko hili la pili hazikubainika mara moja.Waziri Mkuu Ariel Henry alifika eneo la mkasa kwa ndege kukagua uharibifu na kutangaza hali ya hatari kwa mwezi mmoja.

Tetemeko hilo pia lilisababisha uharibifu mkubwa katika mji ulio karibu wa Les Cayes, ambako nyumba ziliporomoka. Vilevile, lilifika hadi nchi za Cuba na Jamaica.

“Niliona miili ikitolewa kwenye vifusi, majeruhi na watu ambao pengine walikufa. Kila nilipopitia nilisikia vilio vya uchungu,” alisema mkazi wa Les Cayes, Jean Marie Simon, 38.

Alikuwa sokoni tetemeko hilo lilipotokea na akakimbia nyumbani kubaini iwapo familia yake ilikuwa salama.

Mkewe na watoto wao wawili walikuwa bafuni wakioga ardhi ilipotetemeka na wakakimbia nje muda mfupi kabla sehemu ya mbele ya nyumba yao kuporomoka.

Video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha raia wakisaidia wenzao kutoka vifusi.Umati wa watu pia walikuwa wakisubiri matibabu katika hospitali zilizolemewa na idadi kubwa ya majeruhi.

Tetemeko hilo lilitokea mwezi mmoja baada ya kuuawa kwa Rais Jovenel Moise. Pia linajiri wakati raia wengi wa Haiti wanakabiliwa na njaa, pamoja na sekta ya afya iliyolemazwa na janga la virusi vya corona.

Wakazi wa maeneo kadhaa ya Cuba na Jamaica walisema walishtushwa na tetemeko hilo japo hakukuwa na ripoti za uharibifu, vifo au majeruhi.

Rais wa Amerika Joe Biden alisema aliagiza nchi yake kutuma misaada Haiti na akamteua Samantha Power, msimamizi wa shirika la misaada la nchi hiyo kushirikisha juhudi hizo.

Rais wa Mexico Andres Manuel Lopez Obrador pia alisema atatumia misaada katika nchi hiyo.

You can share this post!

Yaibuka Wizara ya Utalii imemumunya mabilioni ya pesa za...

WANTO WARUI: Serikali iwape vijana mazingira bora kuundia...