• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 1:22 PM
UN yalaani mapinduzi Guinea

UN yalaani mapinduzi Guinea

Na MASHIRIKA

CONAKRY, GUINEA

KATIBU mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres, Jumapili alilaani vikali mapinduzi yaliyotekelezwa nchini Guinea na kuwataka wanajeshi waasi wamwachilie huru Rais Alpha Conde mara moja.

Kulingana na ripoti za vyombo habari, hatima ya rais huyo haijulikani baada ya video iliyosambazwa mitandaoni ikimwonyesha akiwa amezingirwa na wanajeshi waliodai wametwaa mamlaka.

Walionekana katika runinga ya kitaifa wakidai kuwa wamevunja serikali na kusambaratisha Katiba ya Guinea.

Awali Wizara ya Ulinzi ilikuwa imesema kuwa jaribio la mapinduzi ya kijeshi lilikuwa limezimwa na wanajeshi watiifu na walinzi wa rais.

Hii ilifuatia ufyatulianaji wa risasi uliotokea karibu na Ikulu ya Rais majira ya asubuhi katika jiji kuu, Conakry.

Kwenye ujumbe kupitia Twitter Guterres alilaani vikali matukio hayo nchini Guinea.

“Binafsi nafuatilia hali nchini Guinea kwa ukaribu. Nalaani vikali kutwaliwa kwa serikali kwa nguvu ya bunduki na ninahimiza kwamba Rais Alpha Conde aachiliwe huru haraka,” Guterres akasema.

Vile vile, Umoja wa Afrika (AU) na Jumiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) zilishutumu hatua hiyo iliyoonekana kama mapinduzi na kutaka Rais Conde aachiliwe huru.

Kwenye taarifa, ECOWAS ilisema hatua hiyo inaenda kinyume na mkataba wake kuhusu Demokrasia na Utawala Bora na kutaka utawala wa kikatiba urejeshwe nchini Guinea.

Tafsiri: CHARLES WASONGA

You can share this post!

Italia watoka sare na Uswisi na kufikia rekodi ya Brazil ya...

Mutua ataka wizara ikomeshe mtindo wa wanafunzi kufika...