• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 12:05 PM
Walioangamia kwenye tetemeko wafika 8,100

Walioangamia kwenye tetemeko wafika 8,100

ADANA, UTURUKI

IDADI ya wahanga walioangamia kwenye tetemeko kubwa la ardhi Kaskazini Mashariki mwa Syria na Uturuki imefika 8,100, maafisa walisema Jumanne jioni.

Hii ni baada ya waliojeruhiwa kufa na waokoaji kutoa miili zaidi chini ya vifusi vya majengo. Nchini Uturuki Makamu wa Rais Fuat Otkay alisema idadi jumla ya vifo ilikuwa 5,894 huku Syria ikirekodi vifo zaidi ya 2,270.

Watu zaidi ya 34,000 wamejeruhiwa nchini Uturuki huku 3,700 wakijeruhiwa nchini Syria. Takwimu za Syria zinarekodiwa na Wizara ya Afya katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali huku shirika la White Helmets likiangazia takwimu katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi.

Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kwamba huenda idadi ya waliokufa ikawa mara nane ya idadi inayojulikana kwa sasa.

Wizara ya Afya ya Uturuki ilisema kuwa magari ya kubebea wagonjwa 813 yamepelekwa katika maeneo yaliyoathirika, na vikundi maalum vya huduma za dharura zaidi ya 220 kuambatana na magari hayo.

Tetemeko hilo lenye ukubwa wa kiwango cha 7.8 kwenye vipimo vya Ritcher lilibomoa majengo mengi.

Tetemeko hilo liliitikisa sehemu ya katikati mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria alfajiri Jumatatu, na kufuatiwa na jingine dakika 10 baadaye, likiharibu vibaya miundombinu katika miji 12.

Kufuatia maafa makubwa yaliyotokana na tetemeko la ardhi nchini Uturuki na Syria, mataifa mbalimbali duniani yameanza kupeleka misaada katika maeneo mbalimbali.

Amerika inaratibu msaada wake katika shughuli za kuwaokoa waathiriwa na kusambaza msaada wa kibinadamu.

Muungano wa Ulaya (EU) unatumia mfumo wake wa kidijitali kuchora ramani za operesheni za kuwaokoa waathiriwa, huku mataifa 13 yakiahidi msaada kwa Uturuki na Syria.

Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani ilisema nchi hiyo imetoa msaada wake chini ya Umoja wa Ulaya, ikiwemo majenereta, mahema, mablanketi na vifaa  vingine.

Madaktari pia wametumwa Uturuki ili kusaidia katika mchakato wa kuwapa waathiriwa huduma za kimatibabu.

Kyriakos Mitsotakis, Waziri mkuu wa Ugiriki ambaye nchi yake imekuwa katika mgogoro wa muda mrefu na Uturuki kufuatia masuala ya kitamaduni ameahidi pia kupeleka msaada wake kwa taifa hilo jirani.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, Filipo Grand, ametoa wito kwa mataifa mengine kushikana mkono ili kusaidia Uturuki na Syria.

Uturuki ni miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa zikikumbwa na matetemeko ya ardhi mara kwa mara, ambapo mwaka 1999 watu 17,000 walikufa kutokana na tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.6 kwenye vipimo vya Ritcher.

Mwaka wa 2011, watu 500 walipoteza maisha yao baada ya tetemeko la ardhi kutokea katika mji wa Van.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Wakenya 8.8 milioni walemewa kulipa ada...

Madiwani watano wa Azimio wapata afueni

T L