• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 8:50 AM
Wasiwasi wazidi katika kiwanda cha nyuklia

Wasiwasi wazidi katika kiwanda cha nyuklia

NA MASHIRIKA

KYIV, UKRAINE

MATAIFA ya Magharibi yamesisitiza kuhusu haja ya “kuimarishwa kwa usalama” wa vituo vya nuklia vinavyotishiwa na vita vinavyoendelea nchini Ukraine.

Hapo Jumapili, mataifa ya Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Amerika, yalisisitiza kuwa kushambuliwa kwa vituo hivyo “kunahatarisha usalama wa dunia nzima.”

Kwenye mazungumzo ya simu Jumapili, viongozi wa mataifa hayo manne walisema wataendelea kuiunga mkono Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi.

Urusi na Ukraine zimekuwa zikilaumiana kuhusu mashambulio ambayo yamekuwa yakiendeshwa dhidi ya kituo cha nuklia cha Zaphorisia, kinachoshikiliwa na Urusi.

Wadadisi wanasema kuwa huenda lawama hizo zikaleta mgogoro mkubwa duniani, hasa ikiwa miale hatari katika kituo hicho italipuka na kuanza kuenea.

Wakati huo huo, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amewarai raia wa taifa hilo kuchukua tahadhari, wanapojitayarisha kusherehekea Siku ya Uhuru.

“Huenda Urusi ikajaribu kufanya shambulio hatari dhidi yetu,” akasema, kwenye hotuba aliyotoa wikendi.

“Moja ya lengo kuu la adui yetu ni kutushambulia na kutuvuruga kwa namna yoyote ile. Hata hivyo, lazima tujitolee vilivyo kukabili uvamizi wa aina yoyote ile,” akasema.

Ukraine inalenga kuadhimisha Siku yake ya Uhuru hapo kesho.

Maadhimisho hayo pia yatafikisha miezi sita tangu Urusi kulivamia taifa hilo.

Vita hivyo ndivyo vilijadiliwa pakubwa na Jumapili na Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, Rais Joe Biden (Amerika), Rais Emmanuel Macron (Ufaransa) na Waziri Mkuu wa Ujerumani Olaf Scholz.

Kwenye mazungumzo yao, walivirai vikosi katika pande zote mbili kuchukua tahadhari wanapoendesha mashambulio karibu na kituo cha nuklia cha Zaphorisia.

Kituo hicho kiko kusini kwa Ukraine, ambapo mashambulio karibu nacho yamezua wasiwasi wa kuzuka kwa mlipuko wa miale ya nuklia kama ule uliotokea mnamo 1986 katika kituo cha Chernobyl.

Viongozi hao walikumbatia mkataba ulioungwa mkono na Rais Vladimir Putin, Ijumaa, kuwaruhusu waangalizi wa Umoja wa Mataifa (UN) kukitembelea kituo hicho siku kadhaa zijazo.

Viongozi hao walisema “wamekubali kuiunga mkono Ukraine kwenye juhudi zake kujilinda dhidi ya mashambulio ya Urusi.”

Jumapili, Ukraine iliripoti mashambulio zaidi kutoka kwa Urusi, hasa katika mji wa Nikopol, ulio karibu na kituo cha nuklia cha Zaphorisia.

Jumamosi, shambulio jingine la droni lililenga msafara wa meli za Urusi katika bahari ya Black Sea, katika mji wa Sevastopol.

Hata hivyo, vikosi vya Urusi vilisema vilifaulu kuidungua droni hiyo.

Mapema mwezi huu, ndege tisa za kivita za Urusi ziliharibiwa vibaya kwenye kituo kimoja cha kijeshi, kilicho eneo la Crimea, lililojitenga na Ukraine.

Urusi ilichukua udhibiti wa eneo hilo mnamo 2014, baada ya kulitenga kutoka kwa Ukraine.

Hata hivyo, Ukraine imeapa kuchukua udhibiti wake tena.

  • Tags

You can share this post!

Kwale wakataa suti na kuchagua mseto

Kivutha Kibwana kushirikiana na Kenya Kwanza

T L