• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 8:55 PM
Kivutha Kibwana kushirikiana na Kenya Kwanza

Kivutha Kibwana kushirikiana na Kenya Kwanza

NA SAMMY WAWERU

GAVANA wa Makueni anayeondoka Kivutha Kibwana ametangaza kushirikiana na kambi ya Kenya Kwanza.

Tangazo hilo limetolewa Jumanne na Rais mteule, William Ruto.

Kwenye chapisho katika kurasa zake za mitandao ya kijamii, Dkt Ruto amesema Prof Kibwana atajiunga na kikosi cha mawakili wake kutetea ushindi wake aliopata katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Wiki iliyopita, mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Bw Wafula Chebukati alimtangaza Ruto ambaye amehudumu kama naibu rais kati ya 2013 – 2022, mshindi katika kinyang’anyiro cha urais.

Ushindi wake hata hivyo umepingwa na kinara wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga.

Bw Odinga aliwasilisha Jumatatu kesi katika mahakama ya upeo, ya juu zaidi nchini akitaka ushindi wa Ruto ufutiliwe mbali.

Kwa ushirikiano na baadhi ya wanaotilia shaka ushindi huo, Odinga anataka mitambo ya Kiems ikaguliwe, kura zihesabiwe upya kati ya matakwa mengine, akidai kulikuwa na wizi wa kura.

“Gavana wa Makueni (akimaanisha anayeondoka), atajiunga na kikosi cha wanasheria wa Kenya Kwanza katika kesi ya kupinga matokeo ya urais inayoendelea,” Dkt Ruto akaandika, akiridhia hatua ya Prof Kibwana kuingia katika kambi yake.

Alisema uamuzi wa gavana huyo utasaidia kuendeleza ajenda za muungano wa Kenya Kwanza kuboresha taifa.

Maandiko ya Ruto yaliandamana na picha zake na Kibwana, na baadhi ya wanasiasa katika makazi yake rasmi, ya serikali.

Prof Kibwana ndiye kiongozi wa Muungano Development Movement Party (MDM), na amehudumu mihula miwili kama gavana wa Makueni.

Katika uchaguzi mkuu, aliunga mkono kuchaguliwa kwa Bw Odinga.

  • Tags

You can share this post!

Wasiwasi wazidi katika kiwanda cha nyuklia

BENSON MATHEKA: Kenya Kwanza haifai kusuta Azimio kwenda...

T L