• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
WHO yatangaza homa ya nyani kuwa janga

WHO yatangaza homa ya nyani kuwa janga

NA XINHUA

GENEVA, USWISI

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limetangaza maradhi ya homa ya nyani kuwa janga la kimataifa.

Hii ni baada ya maradhi hayo hatari kuthibitishwa katika zaidi ya nchi 70 kote duniani.

Maafisa katika shirika hilo walisema tahadhari hiyo inalenga kuziamsha taasisi na idara za afya katika mataifa husika kuweka juhudi kudhibiti kuenea kwake.

Vile vile, walisema hilo linalenga pia kuyashinikiza mataifa yote kuunganisha juhudi zao ili kuimarisha mikakati ya kudhibiti kusambaa kwake.

WHO ilizishauri serikali katika nchi zote kutoa uhamasisho na mafunzo maalum kwa madaktari katika hospitali zote kuhusu njia za kujilinda wanapowashughulikia watu walioathiriwa na maradhi hayo.

Shirika hilo pia liliyashauri mataifa yote kuwaelimisha raia kuhusu njia za kujilinda, hasa wanapotangamana katika maeneo ya wazi.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Dkt Tedros Adhanom, alitoa tangazo hilo licha ya ukosefu wa makubaliano miongoni mwa wataalamu wanaohudumu katika kamati ya kushughulikia hali za dharura.

Akitoa tangazo hilo kwenye kikao na wanahabari jijini Geneva, Tedros alithibitisha kuwa kamati hiyo ilikosa kuafikiana kuhusu ikiwa wanapaswa kutangaza maradhi hayo kuwa janga la kimataifa au la.

Wanachama sita walimuunga mkono, huku tisa wakipinga uamuzi wake.

“Tuna janga hatari ambalo limesambaa kote duniani kwa haraka kupitia njia mpya za uambukizaji, ambazo hata sisi bado hatujazibaini kikamilifu. Hata hivyo, usambaaji wake wa haraka umefikia kiwango cha kutangazwa kama janga hatari la kiafya,” akasema Tedros.

Akaongeza: “Ninajua kumekuwa na ugumu mkubwa kuhusu uamuzi huu, kwani kulikuwa na hisia tofauti miongoni mwa wanachama.”

VIFO

Tedros alisema kuwa kuna zaidi ya visa 16,000 vya maambukizi katika nchi 75, na vifo vitano.

Mkuu wa kushughulikia hali za dharura katika shirika hilo, Dkt Michael Ryan, alisema kuwa Tedros aliamua kutoa tangazo hilo ili kuhakikisha nchi zote zimechukua tahadhari za kutosha mapema kudhibiti maenezi yake.

Maradhi hayo yamethibitishwa katika baadhi ya sehemu za mataifa ya Kati na Magharibi mwa Afrika kwa miaka kadhaa iliyopita.

Hata hivyo, haikubainika kuhusu ikiwa maradhi hayo yanaweza kuenea katika sehemu zingine duniani hadi Mei 2022.

Wataalamu walibaini virusi hivyo katika baadhi ya sehemu barani Ulaya, Amerika Kaskazini kati ya maeneo mengine.Kufikia sasa, vifo vya maradhi hayo vimeripotiwa barani Afrika, hasa Nigeria na DRC Congo.

Barani Afrika, maradhi hayo huwa yanaambukizwa binadamu na wanyama kama panya. Visa hivyo huwa vichache na havijakuwa vikithibitishwa katika sehemu zingine duniani hadi mwaka huu 2022.

Barani Ulaya, Amerika Kaskazini na kwingineko duniani, maradhi hayo yanaambukizwa baina ya wanadamu.

  • Tags

You can share this post!

Wake wa vigogo wajitosa kupigia debe mirengo yao

Warembo wa Ufaransa wabandua Uholanzi kwenye Euro 2022

T L