• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Warembo wa Ufaransa wabandua Uholanzi kwenye Euro 2022

Warembo wa Ufaransa wabandua Uholanzi kwenye Euro 2022

Na MASHIRIKA

KOCHA Corine Diacre wa Ufaransa amesema vipusa wake “wana kiu ya kuandikisha historia” baada ya kudengua mabingwa watetezi, Uholanzi, kwenye robo-fainali za Euro za wanawake mwaka huu kwa 1-0 mnamo Jumamosi.

Bao la pekee katika pambano hilo lililosakatiwa ugani New York, lilijazwa kimiani na Eve Perisset kupitia penalti iliyotokana na tukio la Dominique Janssen kuchezea Kadidiatou Diani visivyo ndani ya kijisanduku.

Ufaransa wanaokamata nafasi ya tatu duniani, wametinga nusu-fainali za Euro kwa mara ya kwanza baada ya kuaga makala yote matatu yaliyopita katika hatua ya nane-bora.

Warembo hao watamenyana sasa na malkia mara nane, Ujerumani, ugani Milton Keynes mnamo Jumatano, siku moja baada ya wenyeji Uingereza kuvaana na Uswidi uwanjani Bramall Lane. Uswidi waliibuka wa tatu kwenye fainali za Kombe la Dunia 2019 kabla ya kuzoa nishani ya fedha kwenye Olimpiki za Tokyo 2020.

Uholanzi wanaoshikilia nambari nne duniani, walimtegemea sana kipa wao Daphne van Domselaar aliyepangua na kudhibiti zaidi ya makombora 30 aliyoelekezewa na wavamizi wa Ufaransa.

“Juhudi zetu zinaendelea kuzaa matunda. Tuko hapa kuweka historia na tayari tumedhihirisha uwezo wetu. Kila mtu ana motisha tele na tutajituma hadi mwisho wa safari,” akatanguliza Diacre.

“Kundi hili la wachezaji linaridhisha sana. Tunatarajia makuu kutoka kwa warembo hawa wanaozidi kuimarika kila uchao. Tumepiga hatua muhimu mara hii na sasa hakuna kulegeza kamba,” akaongeza.

Uholanzi waliokuwa wanafainali wa Kombe la Dunia 2019, walitawazwa malkia wa Euro mnamo 2017 chini ya kocha Sarina Wiegman ambaye sasa anadhibiti mikoba ya Uingereza.

Ufaransa walifungua kampeni zao za Kundi D kwa ushindi mnono wa 5-1 dhidi ya Italia kabla ya kupepeta Ubelgiji 2-1 na kusajili sare ya 1-1 dhidi ya Iceland. Kwa upande wao, Uholanzi walianza kampeni za Kundi C kwa sare ya 1-1 dhidi ya Uswidi kabla ya kucharaza Ureno 3-2 na kukomoa Uswisi 4-1.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

WHO yatangaza homa ya nyani kuwa janga

‘Jicho la Jahazi’ lilivyogeuka kuwa kitambulisho cha...

T L