• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Wake wa vigogo wajitosa kupigia debe mirengo yao

Wake wa vigogo wajitosa kupigia debe mirengo yao

NA WANDERI KAMAU

KAMPENI za Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9 zinapoendelea kushika kasi, wake wa vigogo wakuu wa kisiasa pia wamejitokeza kuwasaidia kuvumisha azma zao.

Baadhi ya wale ambao wamejitokeza kuwasaidia vigogo hao ni Bi Ida Odinga, Bi Dorcas Gachagua, Bi Rachel Ruto, Dkt Susan Mboya kati ya wengine.

Bi Odinga ni mkewe mwaniaji urais wa Azimio-One Kenya, Bw Raila Odinga, Bi Gachagua ni mkewe mgombea-mwenza wa Naibu Rais William Ruto, Bw Rigathi Gachagua, Bi Ruto akiwa mke wa Dkt Ruto huku Dkt Mboya akiwa mkewe aliyekuwa gavana wa Nairobi, Dkt Evans Kidero.

Tangu Bw Odinga alipoanza kampeni zake za urais Januari, Bi Odinga amekuwa akiandamana naye katika majukwaa tofauti, ambapo amekuwa akiwarai wanawake kujitokeza kumuunga mkono na kumpigia kura Agosti 9.

Kando na kuandamana na Bw Odinga, Ida amekuwa akienda katika baadhi ya maeneo peke yake au akiwa ameandamana na mgombea-mwenza wa Bw Odinga, Bi Martha Karua.

Hapo jana Jumapili, Bi Odinga alikuwa katika Kaunti ya Migori, alikowarai wenyeji kujitokeza kwa wingi kumuunga mkono Bw Odinga.

“Nawarai kujitokeza Agosti 9 kumpigia kura Bw Odinga kuhakikisha kuwa ndiye atakuwa rais wa tano wa Kenya,” akasema Bi Odinga.

Alimsifia Bw Odinga kama kiongozi shupavu na mwenye uwezo kuwasaidia Wakenya kuepuka changamoto za kiuchumi zinazowakabili.

Bi Gachagua naye amekuwa nguzo kuu kwenye kampeni za mumewe na mrengo wa Kenya Kwanza kwa jumla.

Wiki iliyopita, Bi Gachagua alikuwa miongoni mwa waandalizi wakuu wa hafla ya maombi iliyofanyika katika Uwanja wa Kasarani, jijini Nairobi.

Kwenye hafla hiyo, Dkt Ruto na Bw Gachagua waliombewa na kupewa Biblia.

Kwa upande wake, Bi Ruto amekuwa kwenye mstari wa mbele kumpigia debe Dkt Ruto kupitia mikutano ya maombi na kundi la wanawake la Joyful Women Organization (JWO), ambalo ndiye mwanzilishi wake.

Dkt Mboya naye amekuwa akiandamana na Dkt Kidero kwenye mikutano tofauti katika azma yake kuwania ugavana katika Kaunti ya Homa Bay.

Wadadisi wanasema kuwa kujitokeza kwa wanawake wa vigogo hao ni njia moja ya kuwasawiri kama watu wanaoheshimu familia kama msingi wa jamii.

  • Tags

You can share this post!

DCI yapaka tope IEBC kura ikibisha

WHO yatangaza homa ya nyani kuwa janga

T L