• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:50 AM
Wito kwa serikali za nchi za Afrika ziongeze uwekezaji katika mifumo ya afya

Wito kwa serikali za nchi za Afrika ziongeze uwekezaji katika mifumo ya afya

NA PAULINE ONGAJI

KIGALI, Rwanda

MAKALA ya pili ya kongamano la kimataifa kuhusu afya ya umma barani (CPHIA 2022) yalifikia tamati jijini Kigali, Rwanda mnamo Alhamisi wiki jana, huku wito ukitolewa kwa serikali za Afrika kuongeza uwekezaji katika mifumo ya afya katika nchi zao.

Aidha washiriki walitoa wito kwa mataifa ya Afrika na washirika wa kimataifa kuimarisha uzalishaji wa bidhaa za kiafya, kuthibitisha maandalizi ya kukabiliana na dharura za kiafya, vile vile kuwezesha ufikiaji wa huduma ya afya kwa wote.

Kongamano hilo la siku tatu lililoandaliwa kati ya Desemba 13 na 15, 2022, lilihusisha zaidi ya washiriki 2,500 kutoka mataifa 90 barani Afrika na mbali, ikiwa ni pamoja na wakuu wa serikali, wanasayansi wa haiba ya juu, wawakilishi kutoka sekta ya kibinafsi, mashirika ya umma, na mashirika ya afya na ustawi ulimwenguni.

Baadhi ya viongozi wa ngazi za juu na wasemaji walioshiriki kwenye kongamano hili ilikuwa pamoja na Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la afya Duniani, Dkt Chikwe Ihekweazu, Mkurugenzi mkuu msaidizi  wa idara ya uchunguzi wa dharura za kiafya katika shirika la WHO, Dkt Ahmed Ogwell Ouma, Kaimu Mkurugenzi wa kituo cha Afrika cha kudhibiti na kuzuia maradhi barani Afrika (Africa CDC), Bi Winnie Byanyima, Mkurugenzi Mtendaji wa mpango wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukimwi UNAIDS, vile vile maafisa wakuu kutoka wizara ya afya nchini Rwanda.

Sawa na kongamano la mwaka 2021 lililoandaliwa kupitia mtandaoni, pia wakati huu suala la mfumo mpya thabiti wa kiafya barani liliangaziwa, huku washikadau wakipaza sauti ya kuundwa kwa mtazamo mpya unaozipa nchi za Afrika uwezo wa kujiandaa kwa majanga ya kiafya katika siku zijazo.

“Mijadala hii inaonyesha tunachofanya ili kutimiza mfumo mpya wa afya barani na mazungumzo yetu yameonyesha kwamba tumepiga hatua kubwa tangu uzinduzi wa mkondo mpya wa afya miaka miwili iliyopita, lakini bado kuna mengi ya kufanya,” alisema Dkt Ogwell.

Katika kongamano hilo ushirika muhimu uliundwa ili kuangazia masuala ya kiafya barani. Kwa mfano mashirika ya Africa CDC na Medicines for Malaria Venture (MMV), yalitia saini mkataba wa makubaliano ili kwa pamoja kuwezesha ufikiaji wa dawa bora za kupambana na malaria, na hivyo kuimarisha matumizi na matokeo ya bidhaa za kiafya ambazo tayari iko barani.

Ushirikiano huu unanuiwa kusaidia mataifa wanachama wa Muungano wa Afrika kuimarisha uzalishaji wa chanjo kwa kuimarisha uwezo uliopo, na kuunda miundomsingi mipya ya kuwezesha uzalishaji bidhaa za kutibu malaria hapa barani.

Kongamano la CPHIA 2022 lilihusisha vikao mbali mbali vilivyoangazia changamoto kuu za kiafya zinazolikumbwa bara hili, ikiwa ni pamoja na mzigo wa mkurupuko wa maradhi yanayoambukizwa, magonjwa yasiyoambukizwa, afya ya akili, mchango wa wanawake katika afya ya umma na uvumbuzi wa kiteknolojia na kidijitali, miongoni mwa masuala mengine.

Hatimaye, Muungano wa Afrika na Africa CDC zilitangaza kwamba kongamano la kimataifa kuhusu afya ya umma barani (CPHIA 2023) litaandaliwa kwa ushirikiano na Wizara ya Afya ya Zambia, jijini Lusaka. ?

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Messi kuendelea kuchezea...

Gretsa kuhamisha makao kutoka Thika hadi Makuyu

T L