• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Afafanua umuhimu wa kuzingatia kilimo asilia kwa kudumisha udongo

Afafanua umuhimu wa kuzingatia kilimo asilia kwa kudumisha udongo

NA SAMMY WAWERU  

KATIKA shamba la Sam Nderitu lililoko eneo la Muguga, Thika lina karibu kila mmea unaozalisha chakula. 

Kuanzia mseto wa matunda, mboga, viungo vya mapishi, nafaka; mahindi na maharagwe, maua na miti dawa, ikiwa orodha ya mimea chache tu kutaja.

Nderitu, ni mwasisi wa Grow Bio Intensive Agriculture Centre of Kenya (G-BIACK), kituo kinachotumika kutoa mafunzo ya mifumo ya kilimoasilia kuzalisha chakula.

Msingi wa mafunzo hayo unaanzia utafiti wa udongo, ndio Agro ecology kwa Kiingereza.

Huku Kenya ikiorodheshwa na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO), kama miongoni mwa nchi zilizolemewa na athari hasi za mabadiliko ya tabianchi, Nderitu anaamini suluhu itapatikana kwa kuangazia udongo.

Hatua hiyo itafanikishwa kwa wakulima kurejelea mifumo asilia kukuza chakula, anaungama.

“Tukikwepa kabisa matumizi ya mbolea, fatailaza na pembejeo zenye kemikali, utakuwa mwanzo wa kurejesha hadhi ya mazingira yetu ambayo yanazidi kumenywa na tabianchi,” Nderitu anasema.

Akiwa mtaalamu wa masuala ya kilimo, hasa udongo, ni kwa sababu hiyo Nderitu amejiunga na dau kuangazia kero ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Alianzisha G-BIACK 2008 akiwa na lengo la kuangazia changamoto za uhaba wa chakula zinazong’ata wakazi na jamii ya Gatuanyaga, Thika anakoishi.

Sam Nderitu, mwanzilishi Grow Bio Intensive Agriculture Centre of Kenya (G-BIACK), kituo kinachotoa mafunzo ya kilimoasilia Muguga, Thika, ni mtaalamu wa udongo, pichani, akielezea kuhusu uundaji wa mboleaasilia. PICHA|SAMMY WAWERU

Anasema, inasikitisha kuona wanalima ila wanachozalisha ni kiduchu na kutia msumari moto kwenye kidonda kinachouguza hutumia fatalaiza na dawa zenye kemikali dhidi ya wadudu na magonjwa.

Kando na kuathiri mazingira, pembejeo zenye kemikali ndio chanzo cha maradhi yanayohusishwa na chakula kama vile Saratani – Kansa.

G-BIACK imekalia kipande cha ardhi chenye ukubwa wa jumla ekari mbili ingawa anasema ekari moja na nusu ndiyo ngome ya maajabu anayofanya kuhamasisha haja ya kurejelea kilimoasilia.

Kituo hicho kikiwa kwenye mazingira tulivu, unapoingia utakaribishwa na majengo yanayositiri ofisi mbalimbali, maghala ya kuhifadhi mseto wa mbegu za nafaka, na pia maabara.

Anafichua kwamba ana zaidi ya aina 400 za mbegu za mimea, kwenye bohari lake.

Aidha, amegawanya shamba lake kiasi kwamba kila mmea aliozamia unapata nafasi.

Kipo kiunga cha mimea ambayo ni dawa asilia, viungio vya vinywaji, vivungulio (greenhouse), dimbwi la samaki, vizimba vya kuku, makao ya mifugo, na eneo maalum kuunda mboleaasilia.

Aidha, hutengeneza mbolea kama vile Vermicomposting (masalia ya mimea, kinyesi cha mifugo na vimelea – minyoo), bokashi (maganda ya mimea kama mpunga), ya majani na matawi na vilevile ya mifugo.

“Inapaswa kuiva kabisa, ili iwe yenye manufaa shambani,” Nderitu asisitiza.

Sam Nderitu anatumia viungio kama vitunguu kukabiliana na kero ya wadudu. PICHA|SAMMY WAWERU

Cha kuridhisha zaidi, ni anavyofuga samaki kwani kidimbwi sehemu moja – kona, ina zizi la kuku, kinyesi cha ndege hao kikielekezwa majini ili kukuza mmea maalum aina ya Azolla.

Azolla ni mmea wenye chanzo cha virutubisho vya Protini na bora kulisha samaki na kuku.

“Agro ekolojia ni mfumo ambapo hakuna chochote kinachotoka nje ya shamba la mkulima na hakuna kinachopotea, kila zao na bidhaa zina thamani. Mfano, kinyesi kinatumika kulima na mazao yanayovunwa yanalishwa mifugo. Kinyesi chake kigeuzwe mbolea,” akasema wakati wa mahojiano na Akilimali Dijitali shambani mwake.

Ikikadiriwa karibu asilimia 70 ya athari za mabadiliko ya tabianchi zinatokana na mienendo na tabia za binadamu, Nderitu alisema umewadia wakati mjadala kurejesha hadhi ya udongo utiliwe maanani.

“Kero ya njaa na uhaba wa chakula, itaangaziwa tukiepuka matumizi ya pembejeo zenye kemikali na badala yake tukumbatie mifumo asilia kuzalisha mazao,” akahimiza mdau huyo.

Mseto wa mbegu za mimea anazozalisha Sam Nderitu. PICHA|SAMMY WAWERU

Takwimu za KNBS za hivi punde, zinaonye Wakenya wapatao milioni 5.5, wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula – njaa.

“Robo ekari inatosha mkulima kukuza aina yote ya mimea, na kujitosheleza chakula na kimapato,” Nderitu anaamini, akisema utafiti aliofanya kupitia kituo chake unatia muhuri kauli hiyo.

Huduma zake akisambaza katika Kaunti ya Kiambu, Machakos na Murang’a, anafichua kwamba tangu azindue G-BIACK ametoa mafunzo kwa karibu wakulima 15, 000, kufikia 2030 akilenga kuhamasisha zaidi ya wakulima 30, 000 tija za kilimoasilia.

Janga la Covid-19 lilipotua nchini, Nderitu anasema aliweza kufikia zaidi ya wakulima 2, 800.

Kenya na ulimwengu, hata hivyo, sasa ni huru dhidi ya ugonjwa huo uliosababishwa na virusi vya Corona.

 

  • Tags

You can share this post!

Polisi wamsaka anayeshukiwa kuua rafikiye kwa sababu ya...

Afrika Kusini yapiga kura ya kuvunja uhusiano na Israel kwa...

T L