• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:58 PM
PATA USHAURI WA DKT FLO: Gesi tele tumboni huletwa na nini?

PATA USHAURI WA DKT FLO: Gesi tele tumboni huletwa na nini?

Mpendwa Daktari,

Nimekuwa nikikumbwa na tatizo la gesi nyingi tumboni na kuteuka kila wakati. Hili ni tatizo lipi la kiafya?

Caroline, Nairobi

Mpendwa Caroline,

Kuwa na gesi nyingi tumboni inafahamika kama kuvimba tumbo. Hii ni hali ambapo unahisi umeshiba, unakosa starehe na huenda tumbo likaonekana kubwa kuliko kawaida.

Hali hii yaweza sababishwa na kula chakula kupindukia, kula kwa kasi, kula vyakula vyenye mafuta mengi, kunywa kinywaji kwa kutumia mrija, kutafuna chingamu na kunywa vinywaji vilivyo na dioksidi ya kaboni kama vile soda.

Kuna baadhi ya vyakula ambavyo pia vyaweza sababisha gesi tumboni kama vile maharagwe, dengu, na nafaka zingine jamii ya maharagwe, aina mbalimbali za kabichi, koliflawa, vilevile baadhi ya vikoleza utamu kama vile sorbitol.

Kuna watu walio na mzio wa lactose wanaokumbwa na matatizo ya kumeng’enya maziwa hivyo kula bidhaa zake kwaweza sababisha gesi tumboni.

Kuvuta sigara pia kwaweza sababisha tatizo hili.

Kiwango cha juu cha gesi tumboni chaweza kuletwa pia na maambukizi kama vile; amoebiasis, H.pylori, hyperacidity, Irritable Bowel Syndrome, kushindwa kumeng’enya chakula, mzio wa vyakula, maradhi yanayosababisha kuvimba kwa ukuta wa ndani ya utumbo, utumbo kuziba, matatizo ya misuli ya utumbo vilevile matatizo mengine ya ogani kama vile figo, ini au wengu.

Wakati mwingine ingawaje ni nadra, hali hii yaweza sababishwa na aina mbalimbali za kansa za fupanyonga.

Ili kudhibiti hali hii, kula polepole, kula viwango vidogo vya vyakula, epuka vyakula vyenye mafuta mengi na vyakula vingine vinavyoongeza gesi tumboni.

Unaweza unda shajara ya chakula ili kurekodi unachokula kila siku na kufuatilia ishara na hivyo kutambua ni vyakula gani vinavyochochea hali hii.

Aidha unaweza tumia tembe za simethicone ili kupunguza gesi tumboni. Pia kuna baadhi ya dawa ambazo husaidia kuvunjavunja chembechembe za sukari katika maharagwe na mboga, na hivyo kupunguza gesi.

Hata hivyo, litakuwa jambo la busara kumuona daktari ili ufanyiwe uchunguzi wa kinyesi miongoni mwa zingine muhimu kutambua tatizo na kupata matibabu.

Mpendwa Daktari,

Nitakabiliana vipi na selulaiti kwenye mapaja yangu?

Jane, Mombasa

Mpendwa Jane,

Selulaiti ni uvimbe na vibonyo kwenye ngozi hasa katika sehemu za mapaja, kiuno, makalio na tumbo, japo wakati mwingine hupatikana katika sehemu nyingine za mwili.

Selulaiti hujiunda kutokana na tishu unganishi na seli za mafuta chini ya ngozi.

Hujitokeza miongoni mwa kati ya asilimia 80 na asilimia 90 ya wanawake walio na zaidi ya umri wa miaka 21, japo wakati mwingine zaweza jitokeza mapema.

Hali hii huwakumba sana wanawake zaidi ya wanaume kutokana na tofauti ya mpangilio wa tishu unganishi na tishu za mafuta chini ya ngozi.

Masuala yanayochangia hali hii ni pamoja na umri mkubwa, mabadiliko ya kihomoni, jeni, uvutaji sigara, chakula kilicho na viwango vya juu vya uwanga na vidogo vya nyuzi, kutofanya mazoezi, mtindo wa maisha unaohusisha kukaa chini kwa muda mrefu na kuvalia nguo za ndani zinazobana ambazo huathiri mzunguko wa damu mwilini.

Selulaiti honekana zaidi kutokana na uzani mzito, japo watu walio na uzani wastani au wa chini pia huathirika. Hazina madhara yoyote japo huathiri mwonekano.

Haziwezi tibiwa kikamilifu kwani ni suala la muundo wa tishu zilizo chini ya ngozi. Kuna tiba mbalimbali ambazo zaweza tolewa na mtaalamu wa ngozi au daktari wa upasuaji wa kimapambo, lakini mara nyingi taratibu hizi huleta matokeo madogo au kukosa kuleta matokeo kabisa.

Kumbuka kwamba hata endapo kutakuwa na matokeo, hayatakuwa ya kudumu.

Mbinu za kukabiliana na tatizo hili ni pamoja na kukanda sehemu zilizoathirika, kuvalia mavazi ya kugandamiza, krimu, matibabu ya laser, acoustic wave therapy, micro-surgery, carbon dioxide therapy, radiotherapy, liposuction miongoni mwa mbinu nyinginezo.

Selulaiti haiwezi zuiwa au kuondolewa kabisa. Ili kuimarisha mwonekano, dumisha lishe bora, fanya mazoezi kila mara (hii husaidia kuunda misuli na kukaza ngozi), usivute sigara, chua sehemu iliyoathirika ili kuimarisha mzunguko wa damu, kunywa maji kwa wingi na udumishe uzani ufaao.

Epuka mbinu za kupunguza uzani kwa kasi ili kuzuia ngozi kunining’inia.

You can share this post!

ODONGO: Wanaotaka Junet atupwe nje na Raila wana wivu tu

Polisi watahadharishwa kuwaomba raia ‘mafuta’

T L