• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Polisi watahadharishwa kuwaomba raia ‘mafuta’

Polisi watahadharishwa kuwaomba raia ‘mafuta’

Na LEONARD ONYANGO

INSPEKTA Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai ameonya maafisa wa polisi wenye mazoea ya kushinikiza watu kununua mafuta ya gari ili kwenda katika eneo la tukio.

Inspekta Jenerali alisema kwamba polisi wanaotaka kununuliwa mafuta au kupewa fedha wanakiuka sheria na watakaopatikana na hatia wataadhibiwa vikali.

Bw Mutyambai aliyekuwa akizungumza kupitia ukumbi wa #EngageTheIG kwenye mtandao wa Twitter, alitoa onyo hilo baada ya Wakenya kulalamika kwamba kumekuwa na ongezeko la visa vya maafisa wa polisi kuomba mafuta au hongo wanaporipoti visa vya uhalifu.

“Maafisa wa polisi wanakuomba Sh5,000 kwenda kukamata mhalifu aliyekuibia Sh20,000. Baada ya kuwapa, mkiwa njiani wanakuomba tena Sh3,000 za kula nyama choma na Sh2,000 za mkubwa wa kituo. Hata baada ya kutoa hela hizo mwizi hapatikani,” akalalama Bw Kinuthia Magera, mtumiaji wa Twitter.

Bi Mercy Okumu alielezea namna alivyonunulia maafisa wa polisi wa eneo la Ngong, Kaunti ya Kajiado, mafuta ya Sh3,000 kumsaidia kumsaka mhalifu aliyekuwa amemtapeli fedha zake lakini mshukiwa hajawahi kukamatwa mwaka mmoja baadaye.

“Wananchi hawafai kununua mafuta ya gari au kutoa hongo ili kupata huduma za polisi. Jukumu la wananchi ni kuripoti kisa na kuacha polisi kuchukua hatua. Kuitisha hongo ni kinyume cha sheria,” akasema Bw Mutyambai.

Inspekta Jenerali, hata hivyo, hakusema hatua ambayo mtu anafaa kuchukua iwapo maafisa wake watamtaka kuwanunulia mafuta au kutoa hongo ili kumhudumiwa.

Bw Mutyambai pia alionya maafisa wa polisi walio na mazoea ya kutembea katika maduka ya kuuza pombe wakichukua hongo kila siku jioni.Onyo hilo lilifuatia baada ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kudai kwamba maafisa wa Kituo cha Polisi cha Kasarani, jijini Nairobi, wamekuwa wakikusanya hongo kutoka kwa wamiliki wa baa na maduka ya pombe kila siku jioni.

“Usitoe hongo kwa maafisa wa polisi. Vita dhidi ya rushwa ni jukumu la kila Mkenya,” akasema Bw Mutyambai.

Ripoti ya Kitengo cha Kupokea Malalamishi dhidi ya Polisi (IAU) ya 2020 inaonyesha kuwa uchunguzi wa maafisa wanaolalamikiwa huchukua muda mrefu hivyo kuchelewesha haki kwa walalamishi.

Kati ya malalamishi 1043 yaliyowasilishwa kwa IAU dhidi ya polisi mwaka jana, ni asilimia 25 tu ambayo yalifanyiwa uchunguzi kufikia Desemba.

Malalamishi 430 yaliyowasilishwa kwa IAU yalihusihana na utepetevu ambapo maafisa wa polisi walikosa kuchukua hatua baada ya kupokea ripoti za uhalifu.

Malalamishi 132 yalikuwa ya kutoa vitisho na 85 ya kuomba hongo.

You can share this post!

PATA USHAURI WA DKT FLO: Gesi tele tumboni huletwa na nini?

WANGARI: Kongamano kuu la mazingira lizindue viongozi...

T L