• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Kenya kunufaika kupitia mpango wa FAO kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi

Kenya kunufaika kupitia mpango wa FAO kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi

Na SAMMY WAWERU

KENYA ni miongoni mwa mataifa yaliyoteuliwa kutekeleza mradi mpya kuboresha kiwango cha misitu na pia kupata fedha kusaidia kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Uzinduzi wa mpango huo, kulingana na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO – UN), unalenga kuangazia uharibifu wa misitu ili kurejesha hadhi ya mazingira.

Aidha, umeratibiwa kugharimu kima cha Dola 1 milioni, kufuatua mkataba wa makubaliano na nchi ya Uingereza.

Aidha, utawezesha mataifa yaliyochaguliwa kuutekeleza kupata fedha kusaidia kupambana na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi (climate change).

Mbinu zitakazotumika zitaenda sambamba na matakwa yanayohitajika kudumisha usalama wa mazingira.

Mpango huo, Improving Measurement for Payments to Reduce Emissions and Strengthen Sinks (IMPRESS), pia unajumuisha mikakati maalum kudhibiti gesi hatari zinazotoka kwenye viwanda na vivungulio vinavyotumia dawa zenye kemikali.

Kenya kuteuliwa, FAO imesema ni hatua kubwa hasa katika kuiweka machoni pa ulimwengu ambapo nchi zingine zitapata jukwaa la mafunzo jinsi ya kuangazia athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Athari tunazoshuhudia zinahitaji mikakati faafu kulinda misitu na kudhibiti gesi hatari zinazochangia kuharibu mazingira,” akasema Carla Mucavi, mwakilishi wa FAO Kenya akizungumza jijini Nairobi.

Akitambua mchango wa serikali ya Kenya katika kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya anga, Bi Mucavi alisema mradi wa FAO utaiwezesha kutathmini hatua ilizopiga kulinda misitu na miti.

“Serikali itajua inapopaswa kukaza nati katika mdahalo mzima kupambana na mabadiliko ya tabianchi,” akasisitiza.

Tayari Kenya ina mpango wa kulinda misitu, ndio National Forest Monitoring System (NFMS), na FAO itashirikiana na Shirika la Huduma za Misitu Nchini (KFS) kutekeleza IMPRESS.

“Utaainisha mikakati na kufungua mianya ya kupata fedha kulinda misitu na mazingira,” akasema Astrid Agostini, Mratibu kitengo cha Kitaifa Kutathmimini Misitu (NFM) FAO.

Mpango huo umezinduliwa siku chache baada ya Kongamano la Kimataifa Kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) kufanyika Glasgow, Scotland, Uingereza, ambapo viongozi wa mataifa mbalimbali ulimwenguni, Kenya ikiwemo, waliahidi kupiga jeki mikakati kukabili athari.

Athari za tabianchi zinaendelea kutatiza sekta ya kilimo na ufugaji, ambapo mamia na maelfu ya mifugo imeripotiwa kufariki kutokana na makali ya kiangazi katika maeneo kame (ASAL).

Wakazi wa maeneo hayo pia wanakadiria hasara kupoteza mimea na mazao shambani.

You can share this post!

Obure ahusisha Mudavadi na kashfa ya Anglo-Leasing

Uhuru apigia debe Raila kumrithi 2022

T L