• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 3:28 PM
Mama mjamzito avuka mto hatari uliofurika akitafuta hospitali ya kujifungulia

Mama mjamzito avuka mto hatari uliofurika akitafuta hospitali ya kujifungulia

STEPHEN ODUOR

MWANAMKE mjamzito katika Kaunti ya Tana River amewaacha wengi vinywa wazi baada ya kuvuka mto hatari akielekea hospitalini kujifungua.

Bi Sadia Mahamud ana bahati kuwa hai kusimulia alivyovuka kijasiri Mto Galole uliofurika kabla ya kujifungua mtoto wa kiume Mohamed Bilal katika Kituo cha Afya cha Madogo.

“Nilikuwa nimebakisha wiki moja kulingana na ukaguzi wangu wa kliniki hivyo basi nilijua nina muda wa kujiandaa. Lakini ghalfa, mnamo Ijumaa asubuhi, nilianza kujihisi vibaya lakini nikapuuza nikifikiri ni kawaida tu,” anasimulia.

Alimwita mkunga wa kitamaduni kambini ili kumnyoosha viungo na akajihisi vyema kabla ya kurejelea shughuli zake hadi jioni mvua ilipoanza kunyesha tena kwa wingi.

“Nilikuwa nimetulia hemani tukipiga gumzo na kucheka na shangazi yangu nilipohisi uchungu mkali ulionisimamisha. Sijui niliondoka vipi lakini nilijua wakati wa kupata huduma kamili ya matibabu ulikuwa umewadia.”

Alikimbia na kuanza kuvuka mto huo hatari ambao umekatiza maisha ya watu wawili karibu wiki mbili zilizopita, huku shangazi yake akiambatana na rafiki yake wakijitahidi kumfikia.

“Nilikuwa karibu nusu mtoni wakati mwanamume aliyekuwa ng’ambo nyingine aliponiona na kupiga mbizi ili kunisaidia kuvuka. Maji yalikuwa yamenifika kifuani na mawimbi yalikuwa yameanza.”

“Uchungu ulikuwa mkali na maji yalionekana kunituliza hivyo nikafikiri ni bora nikae ndani hadi uishe lakini wanawake walionisindikiza hawakukubali kamwe.”

Wakishirikiana na wanaume, wanawake walimsaidia Bi Mahamud aliyeketi majini huku shingo yake tu ikionekana.

Wanaume walimwinua kumtoa majini huku akipiga mayowe na kuwauma nao wanawake wakimzaba makofi ili kumtuliza.

“Ilikuwa safari ndefu kwetu kwa sababu alikuwa anauma watu na kutupiga mateke na njia pekee ya kukomesha ukaidi huo ni kumtandika vizuri, akatulia. Hizo ndizo sarakasi tunazoshuhudia wanawake wanapojifungua kwa mara ya kwanza,” alieleza mkunga wa kitamaduni kwa jina Eshah Ismail.

Waliendelea kung’ang’ana mwendo uliosalia wa kilomita nane wakitembea kwa sababu hakukuwa na pikipiki barabarani hadi walipowasili katika kituo cha afya.

“Hakukaa sana tulipofika kabla ya kujifungua kitoto kivulana lakini alikuwa amechoka sana hangerejea siku hiyo, kwa hivyo tukasubiri,” anasema.

Bi Ismail, anasema mama na mtoto wake wana bahati kuwa hai kwa sababu kifo kiliwakodolea macho safarini.

Anasema hakuna mtu amewahi kumudu kuvuka mto Lagger akiwa pekee yake ukiwa umefurika hivyo basi alijihatarisha mno kukabili mawimbi akiwa mtoni katikati.

“Sehemu hiyo ina historia ya vifo, wanawake, wanaume na watoto wamesombwa na kupatikana wakiwa wamezikwa mbali, nadhani Mola alikuwa nasi siku hiyo.”

Wanatumai kuwa serikali siku moja itajenga daraja kuwasaidia wakazi kuvuka kirahisi kutoka Kijiji cha Baraka.

Watu zaidi ya 20,000 wameathiriwa na mafuriko Kaunti hiyo.

Mwelekezi wa Shirika la Msalaba Mwekundu Kaunti hiyo, Jerald Bombe, anasema vijiji vinane vinaweza kufikiwa tu kupitia angani hivyo haja ya kupata helikopta.

  • Tags

You can share this post!

Justina Syokau asema anatafuta kijana barobaro bilionea...

Mwendwa asifu programu ya FIFA na CAF kuwapa makocha...

T L