• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Shule yatoa ilani kuhusu apu ya Roblox inayoweka watoto kwenye hatari ya ngono

Shule yatoa ilani kuhusu apu ya Roblox inayoweka watoto kwenye hatari ya ngono

NA LABAAN SHABAAN

MZAZI mmoja ametahadharisha wazazi wengine kuhusu tovuti maarufu ya kutoa mafunzo na michezo ya watoto kwa jina Roblox.

Mzazi huyu aliyepokea barua kutoka kwa shule anakosomea mtoto wake, aliichapisha katika mtandao wa kijamii wa X (awali Twitter) kama ilani ili jamii itahadhari na hatari za grafiki za kingono kwa watoto.

Taifa Leo Dijitali imeona nyaraka zenye mambo ya kuogofya ukizingatia hatari inayowakodolea macho watoto wanaosoma na kujibamba kutumia simu, tarakilishi, ama vifaa vingine vya kidijitali.

Katika barua kwa wazazi, shule hii imeingiwa na hofu kuhusu apu na tovuti ya Roblox ikisema inaingiza wanafunzi katika mambo maovu.

“Wazazi wanahitaji kuwa makini watoto wao wasihusishwe na vipindi vya watu wazima, vikihusisha grafiki na mazungumzo ya ngono, maongezi na watu wasiojulikana wakiwemo wanyanyasaji wa ngono na matangazo ya kibiashara ya kupotosha,” inasema sehemu ya barua iliyosambazwa kwa wazazi ikiwaelekeza wazazi kutoruhusu matumizi ya programu ya Roblox.

“Tunakusihi kuwahimiza watoto watumie tovuti nyingine ya masuala ya elimu wakiwa nyumbani kuhakikisha wako salama mitandaoni na nje ya mitandao,” shule ilihimiza wazazi.

Mmoja wa wazazi waliopakia barua hiyo mitandaoni alionyesha sehemu ya mazungumzo ya watoto wanaotumia apu hiyo wakifanya mawasiliano ya kimapenzi.

Hii ni sehemu ya waraka ulioandikwa na watoto mtandaoni humo:

“Hujambo mpenzi? Unataka kuwa mpenzi wangu? Nakupenda sana. Unapendeza. Unataka uchumba? Utakuwa mpenzi wangu? Tafadhali. Nitakushika sehemu za siri…”

Inaaminika huenda watu wanaojifanya watoto wanaweza kutumia tovuti hizi kuwa jukwaa la kuwanasa na kuwadhulumu watoto kimapenzi.

Malezi ya watoto katika enzi hizi za utandawazi yako katika njia telezi huku wazazi, walezi na walimu wakitakiwa kuwajibika na kuwa macho.

Wito wa walezi kuwa makini unanuiwa kuhifadhi watoto wasitoswe katika mafunzo yasiyofaa.

Mhadhiri katika Idara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Kielimu Chuo Kikuu cha Kenyatta, Dkt Hamisi Babusa, anapigia debe matumizi ya apu hizi.

Dkt Babusa anasema Roblox ni nzuri kwa watoto kufurahia michezo ya tarakilishi kwa sababu hukuza uwezo wa kufikiria na kuwasaidia kutafuta suluhu ya matatizo.

“Kizazi cha sasa kinaishi katika enzi zao na wazazi hawafai kuwazuia kuchangamkia maendeleo ya kiteknolojia,” alieleza mhadhiri akisisitiza wazazi wanafaa kuhakikisha mipangilio ya programu hizi imewekwa kufaa watoto.

“Mzazi anaweza kuunganisha kifaa anachotumia mtoto na simu yake ili kufuatilia mambo anayofanya mtoto wake kwenye mitandao na kwa jinsi hii atakuwa na udhibiti,” anaongeza.

Msomi huyu ambaye ni mwanzilishi wa chaneli ya mtandao wa YouTube, Babusa TV, hutayarisha vipindi vya kuburudisha kwa kuhusisha watoto.

Dkt Babusa huendesha televisheni dijitali inayofunza Kiswahili kwa kutumia nyimbo na hulenga walimu na wanafunzi wa kutoka chekechea hadi gredi ya tatu.

  • Tags

You can share this post!

Wanaume wawili wananitaka, sijui nichague yupi kati yao;...

Kampuni ya Elgon Kenya yatuzwa na Rais Ruto kufuatia...

T L