• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
PENZI LA KIJANJA: Akikuacha, hakuwa wa kwako!

PENZI LA KIJANJA: Akikuacha, hakuwa wa kwako!

NA BENSON MATHEKA

DAMARIS* alitengana na mumewe baada ya kushindwa kuvumilia tofauti zilipozuka baina yao.

Aliolewa na mwanamume mwingine lakini wakaachana na akarudi kwa mumewe wa kwanza ambaye japo shingo upande, alimkubali kwa sababu walikuwa na watoto wawili.

Hata hivyo, baada ya mwaka mmoja, Damaris alimuacha tena na akaenda mjini alikokutana na mwanamume wa tatu, wakaishi pamoja kwa muda hadi juzi alipotaka kurudi kwa mumewe wa kwanza. Mumewe amekataa kumkubali na ameamua kulea pekee yake watoto wake wawili ambao umri wao ni miaka 10 na 12.

Tabia ya Damaris ni sawa na ya Alex*, mwanamume mwenye umri wa miaka 36 ambaye amekuwa akimuacha mkewe na kuoa wanawake wengine kwa muda kisha kuwatema na kumrudia tena.

“Alitorokwa na mke wa nne juzi na akarudi nyumbani. Kwa kuwa ninaishi kwake siwezi kumkataa,” mkewe Cynthia* aliambia Pambo.

Tofauti na uhusiano wa Damaris na mumewe, Cynthia na Alex hawana watoto wakubwa. Mtoto wao wa pekee ana umri wa miaka sita.

Wataalamu wa masuala ya mahusiano wanatahadharisha watu dhidi ya kuvumilia wachumba wanaopenda ufuska.

“Kuna watu wanaopenda kurandaranda hapa na pale wakioa na kuolewa, wasioridhika na kutulia katika ndoa zao. Mtu anayeacha mume au mke wake na kuolewa kisha arudi, ni hatari. Hajui thamani ya ndoa,” asema Lena Kantai, mshauri katika shirika la Big Hearts jijini Nairobi.

Kantai anasema japo wachumba huwa wanatofautiana na kuamua kuachana au mmoja kumuacha mwenzake akishindwa kuvumilia katika ndoa, mtu akiolewa au kuoa baada ya kutengana na mchumba wake na arudi, huwa anamdharau anayemkubali tena katika maisha yake.

“Mtu anayejiheshimu na kuheshimu ndoa akitengana na mume au mke wake, huwa anatulia akiishi peke yake. Akiolewa au kuoa mara kadhaa na arudi kwako, unafaa kuwa makini kabla ya kumkubali kwa sababu anaweza kukutenda tena kwa kuwa anakudharau,” asema.

Pius Musungu, mwanasaikolojia wa kituo cha Maisha Mema, Nairobi, anasema mtu mwenye tabia ya kuruka kutoka ndoa moja au nyingine, huwa na tatizo la kisaikolojia na ni hatari hata kwake binafsi.

“Ukiona mtu anayemuacha mumewe na kwenda kuolewa mara kadhaa na kisha atake kurudi, unafaa kumsaidia kupata huduma za mwanasaikolojia kwa kuwa sio kupenda kwake,” asema.

You can share this post!

Barcelona wajinasia huduma za Adama Traore kutoka Wolves

FATAKI: Penzi likiingia mdudu usikonde dada, jipe shughuli!

T L