• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
FATAKI: Penzi likiingia mdudu usikonde dada, jipe shughuli!

FATAKI: Penzi likiingia mdudu usikonde dada, jipe shughuli!

NA PAULINE ONGAJI

JUMA lililopita nilisoma habari kumhusu bibi mmoja hapa nchini aliyeamua kuwaua wanawe kabla ya yeye mwenyewe kujitia kitanzi.

Kulingana na taarifa hiyo, alifanya hivyo baada ya kugundua kwamba mumewe alikuwa atafuna pembeni.

Kisa hiki kiliibua mjadala mkali mtandaoni huku wengi wakimlaumu kwa kuchukua hatua hiyo, badala ya kuachana na dume hilo mara moja.

Ni rahisi kumlaumu, lakini wengi hawajui kwamba kuna wanawake walionaswa na ndoa kiasi kwamba hawajui wafanye nini nje ya ndoa.

Huyu ni mwanamke ambaye huhisi hawezi katu kuishi bila huyu mwanamume. Hii huwa hatari kwani dume likigundua hili, laweza kukufanyia chochote kile kwani laamini hutabanduka ulipo.

Mbali na hayo, wanawake wengi walio katika uhusiano wa aina hii huwa wamenaswa katika maisha ya kumtegemea mwanamume kwa vyovyote vile. Iwe ni chupi, chumvi au kiberiti, mwanamume ndiye hugharimia, suala linalompokonya uwezo wa kujitegemea maishani pasipo dume hilo.

Kisha kuna huyu binti ambaye baada ya kuolewa, alisahau kila kitu kujihusu – iwe kitaaluma au kielimu na badala yake, maisha yake yalizingira mahitaji ya mumewe. Hapa akitaka kuachwa anahisi kana kwamba anakabwa kooni na maisha yamefika kikomo.

Alafu kuna wale ambao hasira za kutaka kujidhuru baada ya kuachwa hutokana na sababu kuwa walipokuwa katika uhusiano au ndoa, dume lilimtenganisha na jamaa na marafiki, na mambo yanapobadilika, aibu humlemea.

Funzo ni kwamba, usichukulie mapenzi kwa umakini sana. Ni sawa kabisa kumpenda mtu, lakini isiwe kana kwamba asipokuwepo maisha hayataendelea. Huyu ni mtu ambaye umekutana naye mkiwa wakomavu kiumri. Iweje ukubali penzi lake likutawale hadi ushindwe kujidhibiti?

Pia, tunapaswa kujipenda kiasi cha kuondoka pindi mwenzio anapoonyesha tabia zisizokufurahisha mkiwa katika uhusiano. Mara nyingi tabia za mwenzio zitaanza kujitokeza mapema penzi likiwa lingali bichi. Akiwa na jicho la pembeni, bila shaka shingo lake litageuka kila rinda linalopita.

Huo ndio wakati wa mwafaka kuondoka ikiwa hauwezi stahimili kulishwa kwenye sinia moja na wenzio kadhaa, badala ya kudhani kwamba utambadilisha tabia mkishaoana!

You can share this post!

PENZI LA KIJANJA: Akikuacha, hakuwa wa kwako!

BAHARI YA MAPENZI: Haki ya kumiliki mali kati ya wanandoa

T L