• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
MITAMBO: Mtambo unaosaidia wakulima kufunga vitita vya nyasi

MITAMBO: Mtambo unaosaidia wakulima kufunga vitita vya nyasi

NA RICHARD MAOSI

MTAMBO wa baler hutumika kushindilia nyasi na hatimaye kuunda vitita vya nyasi.

Nyasi hizo maarufu kama hay, ni lishe ambayo inaweza kutumika badala ya nyasi za kawaida hususan kwa wakulima wa ng’ombe wa maziwa, wanaotokea maeneo kame, sehemu ambazo kwa kawaida ni nadra kupata malisho.

Aidha mkulima anaweza kusafirisha malisho yake mbali ikizingatiwa kuwa ni mtambo ambao huvuna, kukausha na kupakia nyasi nyanjani sehemu ambazo zina uhaba wa vibarua.

Kulingana na Isaiah Berile kutoka Shirika la Mimea na Mifugo Nchini (KALRO), Lanet, anasema mitambo ya baler huwa imegawanyika katika mifumo mbalimbali kulingana na matumizi.

Kwanza kuna muundo wa baler ambao unaweza kutenganisha makapi kutoka kwenye lishe ya mifugo ili kupata sehemu ya chakula inayohitajika.

“Manufaa yake huwa ni mengi kwa mfano huwasaidia wakulima kupata nafasi ya kutosha inayotumika kuyahifadhi malisho yao,” anasema.

Pili, Berile anasema mtambo wenyewe unaweza kutumika kukamua kitu kiowevu kutoka kwenye malisho ili kuwalisha ndama wachanga ambao hawajakomaa na wanahitaji vitamini kama sehemu ya malisho yao.

Anasema sehemu hii ya mtambo inafahamika kama- Liquid extraction baler.

“Kinyume na aina nyinginezo za mitambo ya shambani ambayo hukata nyasi tu, baler hutumika kukata ngano, pamba au maharagwe ya soya ambayo huchanganywa na molasses,” anasema.

Anasema shughuli ya kuvuna na kutengeneza vitita mbalimbali vya malisho inaweza kugeuzwa kuwa kitega uchumi na hivyo basi kutoa fursa nyingi za ajira kwa wanaohusika.

“Kutokana na hali ya mabadiliko ya hali ya anga nchini, mkulima anaweza kuvuna nyasi zake kisha akazifunga na kuzihifadhi ili kuziuza msimu wa kiangazi,”anaeleza.

Kilimo hiki cha nyasi kinaweza kuendeshwa katika maeneo kame ambayo hushuhudia kiwango kidogo cha mvua, ikizingatiwa kuwa maeneo kame hutoa mazingira mwafaka kwa nyasi kumea.

Kulingana na Berile, endapo mkulima atakumbatia matumizi ya mtambo wa baler , hataingia kwenye gharama nyingi za kuandaa shamba kwa sababu nyasi huwa zinapatikana kwa wingi.

Uchunguzi unaonyesha kuwa biashara ya hay huwa ni nzuri kwani muuzaji anaweza kutengeneza kati ya Sh400-450 kutoka kwa tita moja msimu wa kiangazi. Isitoshe, anasema kuwa maeneo yenye muundo msingi bora kama barabara nzuri, inaweza kusaidia biashara hiyo kunoga kutokana na wepesi wa shughuli za uchukuzi.

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Nyasi maalum inayopatia wafugaji matumaini tele

Gaspo Women kususia mechi dhidi ya Vihiga Queens

T L