• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
Viwanda vya chai vyabaki pweke Murang’a wakulima wakiuza majani mabichi kwa pesa za haraka

Viwanda vya chai vyabaki pweke Murang’a wakulima wakiuza majani mabichi kwa pesa za haraka

KNA na SAMMY WAWERU

BIASHARA ya kuchuuza majanichai mabichi maeneo yanayolimwa zao hilo katika Kaunti ya Murang’a imesababisha baadhi ya viwanda vya Shirika la Kustawisha Sekta ya Chai Nchini (KTDA) kupokea kiwango cha chini cha chai.  

Na kutokana na hilo, uongozi wa kiwanda cha chai cha Gatunguru, Mathioya unalaumu baadhi ya wakulima kwa kuuzia wasagaji wa kibinafsi mazao yao hivyo basi kuchochea hali kuwa mbaya zaidi.

Kwenye mkutano wa kila mwaka wa kiwanda hicho (AGM), uliofanyika majuzi, ilibanika kwamba kiwango cha majanichai yanayopokewa kutoka kwa wakulima 2023 kimeshuka kwa asilimia 7.03 ikilinganishwa na mwaka uliopita, 2022.

Mwenyekiti wa kiwanda hicho, Samson Kaguma alidokeza kwamba data ya 2023 iliyotolewa Juni 30, wakulima wanaokisambazia chai walikipa kilo milioni 18.119 pekee za chai ya kijani (majanichai mabichi), kiwango hicho kikiwa ni mshuko kutoka kilo milioni 19. 48 mwaka 2022.

Bw Kaguma alikashifa vikali tabia za uchuuzaji chai akisema zimefanya kiwanda anachoongoza kuhudumu chini ya kiwango inachopaswa.

“Katika kalenda ya mwaka uliopita, wakulima walichuuza majani chai mabichi na kampuni za kibinafsi ili kupata pesa za haraka,” afisa huyo akalalamika.

Aidha, alisema hatua hiyo inaenda kinyume na mkataba ambao wakulima wametia saini na kiwanda cha Gatunguru.

Mbali na wakulima kuchuuza mazao yao kwa minajili ya mapato ya haraka, Kaguma pia alitaja athari za mabadiliko ya tabianchi kama sababu nyingine ya kiwango cha uzalishaji chai kushuka.

Kabla ya nchi kuanza kupokea mvua mapema 2023, Kenya ilishuhudia janga la ukame lililotajwa kama la kihistoria kuwahi kuonekana kwa muda wa miaka 25 iliyopita.

“Kwa sababu ya mvua kubwa tunayoendelea kupokea, msimu huu tunatarajia mazao bora na mengi. Murang’a, Mathioya tumepata mvua ya kuridhisha,” Bw Kaguma akasema.

Kupunguza gharama, Mwenyekiti huyo wa Kiwanda cha Chai cha Gatunguru alifichua kwamba wamenunua mashine na mtambo wa kisasa kusindika chai.

“Mwaka wa Fedha 2022/2023, gharama ya utendakazi ilikuwa juu. Hata hivyo, itashuka kufuatia mashine ya kisasa tuliyonunua.”

Afisa huyo aliwataka wakulima kutii kanuni zilizowekwa na KTDA, wakati wakitia saini mkataba wa makubaliano.

Alitangaza kwamba kiwanda cha Gatunguru kinaendeleza mikakati kuanza kusaga chai ya hadhi ya juu (orthodox tea), hatua ambayo itasaidia wakulima kutia mfukoni mapato ya kuridhisha.

Baadhi ya viwanda nchini vimeanza kusindika majani chai hayo ya hadhi, jambo ambalo limeonekana kuletea wakulima afueni kimapato.

Kuzima kero ya uchuuzaji wa majanichai mabichi, mwanachama wa Bodi ya Zoni Nambari 3, Chege Kirundi alisisitiza haja ya wakulima kuelezwa kanuni za KTDA wanapotia saini mkataba wa makubaliano.

Alisema wanapaswa kufahamu kuwa ni hatia na haramu kukiuka sheria zilizowekwa.

Wakati huohuo, Bw Kirundi alibaini kwamba kawi inayozalishwa na kiwanda cha Metumi itasambazwa kwa kampuni zingine sita Murang’a ili kuvisaidia kushusha gharama ya utendakazi.

Kawi hiyo inatokana na ushirikiano baina ya viwanda vitatu, vilivyoungana kuanza kuizalisha.

  • Tags

You can share this post!

Kanisa lafungisha ndoa za pamoja kusaidia kupunguza tabia...

Raha ya mjane mchanga wa Kibor wakili akiambia korti...

T L