• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 10:25 PM
Raha ya mjane mchanga wa Kibor wakili akiambia korti anastahili donge alilomegewa kwenye urithi

Raha ya mjane mchanga wa Kibor wakili akiambia korti anastahili donge alilomegewa kwenye urithi

TITUS OMINDE NA FRIDAH OKACHI

Mahakama inayosikiza kesi kuhusu urithi wa mali ya zaidi ya Sh16 bilioni ya marehemu mkulima na mwanasiasa maarufu wa Uasin Gishu Jackson Kibor, imeambiwa marehemu alikuwa ametayarisha wosia uliowasilishwa kortini alipokuwa na akili timamu.

Baadhi ya wanafamilia wa Mzee Kibor wamepinga wosia huo, wakidai si sahihi.

Wamedai marehemu hakuwa sawa kiakili wakati wa maamuzi hayo.

Wakili wa marehemu Mzee Kibor ameiambia mahakama kuwa marehemu alikuwa na akili timamu alipompa maelekezo ya jinsi mali yake itagawiwa wajane na watoto wake.

Wakili Bundotich Korir, alitoa ushahidi siku ya Jumatatu, Novemba 20, 2023 akisisitiza kuwa wosia huo ni dhihirisho halisi jinsi Mzee Kibor alitaka himaya yake igawanywe miongoni mwa wanafamilia.

Bw Korir alieleza hakimu wa Mahakama Kuu Reuben Nyakundi, kuwa kila kitu kilichomo katika wosia huo ilikuwa mapenzi ya kweli ya mteja wake.

Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, iliibuka mjane mdogo wa Mzee Kibor, Eunita Kibor ambaye ni mke wa nne, alikubali wosia huo kinyume na wanafamilia wengine.

Kesi hiyo iliwashirikisha watoto 29 wa tajiri huyo na mama yao mdogo wa kambo, Eunita Kibor.

Wakili huyo aliambia mahakama miezi michache kabla ya kifo cha Mzee Kibor, alimwita kwenye mkutano katika makazi yake ya Elgon View katika mji wa Eldoret na kumwagiza atoe wosia wake kueleza jinsi himaya yake kubwa inavyopaswa kugawanywa miongoni mwa watu wanaomtegemea, wakiwemo watoto aliozaa nje ya ndoa.

Wakili huyo alitupilia mbali madai ya waliopinga kuwa Mzee Kibor hakuwa na akili timamu alipompa mamlaka ya kuandika wosia wake akionyesha namna ya ugawaji miongoni mwa wanafamilia yake.

“Kwa ufahamu wangu, marehemu Kibor alikuwa na akili timamu wakati wosia ulindaliwa na aliweza kuelewa anafanya nini katika suala la ugawaji wa mali yake kwa watoto wake ambao sasa wanapiga,” Korir alisema.

Aliendelea kuambia mahakama Wosia wa Mzee Kibor uliandikwa Februari 27, 2021 na kushuhudiwa na mawakili wawili ambao ni Joseph Kaptich na David Songok.

“Marehemu alitoa maagizo kwamba mimi na mke wake mdogo tuwe watekelezaji pekee wa Wosia wake uliotiwa saini Februari 27, 2021,” alisema.

Mahakama pia ilifahamishwa jinsi marehemu alivyomwalika nyumbani kwake katika kijiji cha Kabenes, Kaunti Ndogo ya Soy mbele ya  wanafamilia wake wa karibu, jamaa, marafiki, viongozi wa kanisa na kisiasa.

Alisema Mzee Kibor alitaka kufichua yaliyomo kwenye wosia wake kwa wanafamilia yake na kumtaka awasomee yaliyomo ndani ya wosia huo ili kila mmoja ajue sehemu yake ya utajiri wake mkubwa.

“Nilikuwa na nakala ya wosia ambayo niliwasomea wanafamilia na wageni wengine waalikwa jinsi marehemu Kibor alivyoagiza ingawa baadhi ya watoto wake walipinga hati hiyo,” alisema Bw Korir.

Tajiri huyo aliyefariki dunia Machi 2022 baada ya kuugua kwa muda mrefu, aliacha wajane watatu – Josephine, Naomi na Eunita Kibor – na watoto 29.

Mkewe wa kwanza, Esther Kibor, alifariki zaidi ya miongo miwili iliyopita.

Mali ya tajiri huyo, inayokadiriwa kuwa Sh16 bilioni, ambayo ni kitovu cha mzozo mkali kati ya watoto wake na mkewe mdogo, ni pamoja na majengo ya biashara katika eneo la biashara kuu la Eldoret, viwanja kadhaa vya kifahari huko Elgon View Estate huko Eldoret, Nakuru, Karen Estate, Nairobi na Nyali huko Mombasa.

Pia aliacha mali zinazohamika, zingine kwenye benki na maelfu ya ekari za mashamba katika kaunti za Uasin Gishu, Trans Nzoia na Nakuru.

Wapinzani 29 katika mzozo huo wa urithi wanawakilishwa na mawakili 10 wakiongozwa na Ken Maiyo na Nixon Koitui, huku mke mdogo wa tajiri huyo Eunita Kibor akiwakilishwa na wakili Karen Chesoo.

Kwenye ombi lao la kupinga wosia huo, walioweka pingamizi ni pamoja na wajane wawili wa marehemu, Josepine na Naomi Kibor, wanaoitaka mahakama kutegua hati hiyo kwa madai kuwa marehemu hakuwa na uwezo wa kutoa uamuzi.

Pia walijitetea kwamba hakuna usawa katika namna mali ya baba yao ilivyogawiwa, huku wakibainisha baadhi yao wamenufaika kwa kupewa zaidi ya wengine katika wosia huo.

Walidai baadhi ya mali alizopewa mke mdogo hazikuwa sehemu ya mali za marehemu kwani walitaka hati hiyo itangazwe kuwa ni batili kupitia taratibu za mahakama.

Hakimu Nyakundi aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 23.

  • Tags

You can share this post!

Viwanda vya chai vyabaki pweke Murang’a wakulima wakiuza...

Wanaonitaka wamesota kama mimi, hawawezi kunisaidia na...

T L