• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 4:26 PM
AKILIMALI: Lishe bora ya mifugo msimu wa kiangazi

AKILIMALI: Lishe bora ya mifugo msimu wa kiangazi

Na RICHARD MAOSI

KUENDESHA ufugaji wa ng’ombe wa maziwa msimu wa kiangazi si rahisi, ikizingatiwa kuwa makali ya ukame huathiri malisho na chemchemi za vyanzo vya maji.

Mvua nyingi nchini hushuhudiwa baina ya Machi na Mei huku msimu wa mvua ya rasharasha ukiwa ni baina ya Oktoba na Disemba kila mwaka.

Ng’ombe wa kukamua wanafaa kupata lishe yenye virutubisho muhimu vya protini, vitamini na madini, kando na kudumisha usafi kila wakati ili kudhibiti maradhi kama vile foot and mouth, mastitis na minyoo.

Akilimali ilitembelea eneo la Maragua, kaunti ya Murang’a ambapo tulikutana na Paul Chege ambaye anafuga ng’ombe watatu wa maziwa aina ya Friesian ndani kwa ndani yaani zero grazing.

Kulingana na Chege, kwa siku moja anaweza kupata zaidi ya lita 100 za maziwa, aghalabu kila ng’ombe akitoa zaidi ya lita 30.

Aidha kwa siku moja anaweza kutengeneza kati ya Sh3000-3500 akisema kuwa siri yake ya ufanisi, ni kuwalisha mifugo wake vyema, kuwapa maji ya kutosha na muda wa kupumzika.

Anasema alipata tajriba ya kufuga ng’ombe kutoka kwa wazazi wake ambao ni wakulima, aidha alitaka kujiendeleza kimaisha baada ya kugundua soko la maziwa lilikuwa kubwa Maragua.

Hata hivyo, anaona kuwa mara nyingi mifugo huwa wanategemea nyasi ambazo hupatikana msimu wa mvua tu, wala wakulima hawana njia nyingine ya kulisha mifugo wao msimu wa kiangazi.

“Hali yenyewe ilinisukuma nikaanza kufanya utafiti kuhusu aina mbalimbali ya lishe ambazo zinaweza kudumu msimu wa kiangazi na ule wa mvua,” akasema.

Alitembelea Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Ufugaji kujifundisha namna ya kubadilisha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa mashinani, na kufanya uwe kilimo biashara

Ndipo alitambua nyasi mpya za kigeni za ziitwazo brachiaria, desmodium, viazi tamu, kama lishe maalum kwa wakulima kutumika msimu wa kiangazi ili kuhakikisha kuwa mifugo hawapungukiwi na malisho .

Ukizitazama aina hii ya nyasi utagundua ni laini na zimekolea rangi ya kijani kibichi. Zina asilimia kubwa ya virutubisho vya protini, kinyume na nyasi za kawaida ambazo madini yake ni haba. Hivyo basi zinaweza kutumika kama lishe mbadala kwa wafugaji msimu wa kiangazi.

Isitoshe anasema lishe ya majani yaliyokaushwa kutokana na mazao ya shambani, inaweza kuhifadhiwa na kutengeneza lishe mbadala ya silage ambayo hulishwa kwa wanyama ikiwa imekaushwa.

Anasema kuwa kama mkulima mdogo amekuwa akitumia silage, inayoundwa kutokana na mabaki ya mahindi na ndizi zinazovunwa na kuhifadhiwa kwenye ghala msimu wa mvua, zikisubiri kutumika msimu wa kiangazi.

“Gharama kubwa ambayo mfugaji anaweza kukumbana nayo ni ile ya kununua lishe,” akasema.

Chege anawashauri wakulima kutengeneza silage kutokana na mabaki ya mimea yakiwa bado na rangi ya kijani kibichi wakati ambapo bado yana virutubishi vya hali ya juu.

Pili anasema kuwa njia hii ni rahisi ikizingatiwa kuwa bado wakulima wengi hawana maarifa ya kutosha, kuhusu brachiaria, desmodium na viazi tamu.

Aina hii ya nyasi za kigeni zinaweza kustawishwa sehemu yeyote, aidha zinaweza kustahimili mazingira makavu, na huweza kuchukua miezi mitatu hivi kukomaa.

“Hulishwa mifugo zikiwa mbichi au wakati mwingine kuhifadhiwa katika ghala na kulishwa kwa mifugo baadaye zikiwa zimekauka,” alisema

Asilia 20 ya virutubisho vyake ni protini, ladha yake ni nzuri, na haiwezi kukabiliwa na maradhi au wadudu. Isitoshe inaweza kukaa shambani kwa miaka isiyopungua 10.

Chege anasema hatua ya kwanza ni pale mkulima anapokusanya mabaki ya mimea kutoka shambani kama vile makapi ya mahindi au napier grass.

Ni jukumu la mkulima kuchagua ni aina ya silage anayotaka kuunda, mara nyingi hii ikitegemea aina ya mimea anayokuza shambani.

Anashauri kuwa atafute sehemu ambayo ni safi na salama ya kuchimba shimo, sehemu hiyo iwe imeinama kidogo ili maji yasije yakatulia endapo mvua ya rasharasha zinaweza kutokea.

Hatimaye Chege hukatakata mchanganyiko wa majani na kuhifadhi ndani ya shimo na kushindilia kisha akafunikwa vyema isije ikakumbana na hewa ya oksijeni.

You can share this post!

AKILIMALI: Ni faida kuongeza viungo thamani

Al Duhail anayochezea ‘Engineer’ Olunga...