• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 AM
AKILIMALI: Ni fundi stadi pale kwa mjengo; kubeba mawe, saruji kunamfaa

AKILIMALI: Ni fundi stadi pale kwa mjengo; kubeba mawe, saruji kunamfaa

Na WINNIE ONYANDO

CHRISTINE Anyango, 24, amejitosa kwa kazi ya ujenzi ambayo kwa muda mrefu imeonekana kushabikiwa zaidi na wanaume.

Lakini mkazi huyu wa Oyugis, Kaunti ya Homa Bay, hakujipata hapo ghafla, ni taaluma ambayo ameisomea.

Anyango alijitosa kwa ujenzi baada ya kukamilisha kozi yake ya Teknolojia ya Ujenzi katika Taasisi ya Ramogi Institute of Advanced Technology mnamo 2019.

Huenda yeye ndiye mwanamke pekee anayejishirikisha na kazi za ujenzi katika eneo hili, kwani katika pitapita zake na pia vibaruani, hajashuhudia wengine.

Anyango anaeleza kuwa ujenzi ni jambo ambalo alilihusudu tangu utotoni, na alivyoendelea kupevuka, alitambua kuwa ndiyo taaluma atakayoifanya ili kuwa na mkondo tofauti na ndugu zake kitaaluma.

“Niliamua kujikita katika taaluma ya ujenzi kwa kuwa ni uwanja ambao wanawake wengi wanaiogopa. Kadhalika nilitaka kuwa wa kipekee,” Anyango anaeleza.

Christine Anyango (kushoto) akifanya kazi. Picha/ Winnie Onyando

Kulingana na ripoti ya kituo cha masuala ya Biashara na Haki za Binadamu, idadi ya wanawake waliopo kwa taaluma ya ujenzi au wanaosomea kozi za sayansi katika vyuo vikuu na taasisi mbalimbali nchini, ni ya chini mno.

Utafiti mwingine ulioangazia wanawake katika mazingira ya ujenzi, ulionyesha kuwa baadhi ya wanawake wanaogopa kozi zinazohusiana na ujenzi, hata ingawaje ni miongoni mwa taaluma zinazokuwa kwa kasi.

Nazo takwimu kutoka Bodi ya Wahandisi Kenya, zinaonyesha kuwa wanawake wanachukua asilimia 10.6 ya waliohitimu kwa uhandisi ambayo ni 1, 519 kati ya jumla ya wahandisi 14,320.

Utafiti huo pia unaonyesha kuwa kati ya wanakandarasi 17, 119 waliosajiliwa na Mamlaka ya Ujenzi ya Kitaifa mnamo Novemba 2020, ni 2,645 tu ambao ni wanawake.

Anyango anatueleza kuwa, alipokuwa akisoma katika taasisi hiyo ya ujenzi, alikuwa mwanafunzi wa kike wa pekee katika darasa lao, wengine 30 wakiwa wanaume.

Japo alikumbwa na changamoto si haba, anasimulia kuwa alijikakamua hadi tamati.

“Kozi ya ujenzi mara nyingi huhitaji ujuzi wa hisabati. Tulijisajili wasichana watatu ila kufikia mwaka wa wa nne, ni mimi tu nilibahatika kufuzu,” anasema.

Sasa hivi, Anyango amebobea katika taaluma ya ujenzi. Ana uwezo wa kuanzisha ujenzi wa nyumba yoyote na kuikamilisha bila tashwishwi yoyote.

Septemba, alifanikiwa kupata kazi kama mkufunzi katika taasisi ya Nyang’iela Vocational Training College.

Anatoa mafunzo kwa wanafunzi 19 katika kozi ya ujenzi.

“Wengi wanapendezwa na kazi ninayoifanya. Bidii yangu imeniwezesha kupata kazi kama mkufunzi katika taasisi hiyo. Kwa yote, namshukuru Mungu.”

Ingawaje kazi hii ina changamoto zake, anaeleza kuwa kwa upande wa mapato, hakosi angalau kuingiza Sh2,000 kwa siku.

“Ni kazi ninayoifurahia na sijawahi kujuta hata siku moja kwa kuamua kufanya kazi hii,” anaongeza.

Anawapa wengi changamoto kutokana na kazi anayoifanya.

Wanaume katika eneo la ujenzi wanamvulia kofia na kumsifu kutokana na bidii yake na kujituma.Wengi wanamsifu kama mwanamke anayejitambua.

Mwanamke mwenye msimamo thabiti na anayetumia nguvu zake kujikimu.

“Anawashinda wengi ambao hulaza damu na kula vya bwerere,” mmoja wa wafanyakazi wenzake anasema.

Changamoto

Tangu ajiunge na kozi hiyo, Anyango amepitia changamoto si haba.

Anasema asilimia 99 katika maeneo ya ujenzi huwa wanaume.

Mwanzoni, anasema alikuwa akiona vigumu sana kutangamana nao.

“Mara nyingi wanaume hunidadisi na kutaka kujua kwa nini nilifanya kozi ngumu kama hii. Kwa muda mrefu, nilishinda nikiwa nimenyamaza kwa kuwa lugha ya wanaume na wanawake ni tofauti. Mada ya mazungumzo pia haikuniruhusu kuchangia gumzo lao. Ila pole pole nikajifunza na kuingiliana nao vizuri,” anaeleza.

“Kwa kawaida, wanawake wanaonekana kama viumbe wanaopenda kujipamba, na wenye kudumisha urembo wao. Kama mwanamke, kazi hunifanya kuchakufa. Kubeba mawe, matofali, saruji, mbao na vifaa vingine vya ujenzi humfanya mtu kuchafuka.”

Anaongeza, “Mara nyingi huwa nabaguliwa kutokana na jinsia yangu kazini. Wengine huninyima kazi na kuwapa wanaume.”

Kulingana na maumbile, wanawake hawana nguvu nyingi ikilinganishwa na wanaume.

Kama mwanamke, Anyango hupata changamoto hasa kubeba saruji, mbao, mabati na vifaa vizito vya ujenzi jambo linalomlazimisha kuomba usaidizi kwa kuwa nguvu zake hazimruhusu.

Pia uchovu ni tatizo lingine katika kazi ya ujenzi, Anyango anaeleza kuwa mara nyingi yeye hurudi nyumbani akiwa na uchovu mwingi sana. Hali hiyo humlazimu kuchukua muda mrefu wa mapumziko.

Hata hivyo, hujaribu kumudu hali kwani anaipenda kazi yake na haina ratiba maalum ya kufuata isipokuwa kujituma.

“Cha muhimu ni kufanya kazi yako kwa ustadi na kujenga ukuruba na wateja wako,” anahimiza.

Vilevile anawashauri wanawake wajifunze kujituma ili kuboresha maisha yao.

“Ukiwa na pesa zako kama mwanamke, utahepa mitego mingi ya wanaume,” anashauri Anyango.

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali iwakinge wananchi maskini

Uhispania wakomesha rekodi ya kutopigwa kwa Italia katika...