• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
AKILIMALI: Pilipili kali inayoogopwa na wenyeji kwa mwasho wake yamletea noti

AKILIMALI: Pilipili kali inayoogopwa na wenyeji kwa mwasho wake yamletea noti

Na CHARLES ONGADI

PILIPILI nyingi zinatambuliwa kwa mwasho wake.

Si kila mtu mwenye uwezo wa kuzitafuna na inabidi utafute maji kwa wingi ikiwa hujazizoea kutuliza ulimi wako, huku zikiwaliza wengine.

Hata hivyo, wenyeji wengi wa Pwani huzitumia kwa wingi katika mapishi yao kuongezea ladha vyakula vyao.

Kuna pilipili ya kienyeji iliyo maarufu miongoni mwa wenyeji wa Pwani hasa maeneo ya Kilifi inayojulikana kama ‘Usinitie Nazi’.

Zipo aina mbili za pilipili aina ya ‘Usinitie Nazi’, kuna yenye rangi nyeupe pepepe na nyekundu.

Ni pilipili yenye umbo dogo lakini inayowasha kiasi cha kwamba unapoitia kwenye chakula cha nazi hakiwezi kulika kwa starehe kutokana na mwasho.

Lakini wenyeji hupenda sana aina hii ya pilipili kutokana na mwasho wake.

Kwa ufupi, ni pilipili iliyo na uwezo wa kupoteza ladha ya chakula kitamu cha nazi kutokana na mwasho wake wa kufanya mtu atokwe na machozi.

Lakini wakulima wengi Pwani hupuuza kilimo cha aina hii ya pilipili kwa dhana kwamba inapatikana kirahisi hasa katika maeneo yaliyo na misitu huku baadhi wakidai ni kilimo kilicho na kazi ya ziada na wala yenyewe haina soko.

Hata hivyo, Bahati Nyanje, mama mwenye watoto sita kutoka Majengo Kanamai, Kaunti ya Kilifi, anakuza pilipili hii.

“Wakulima wengi hapa wamepuuza kilimo cha aina hii ya pilipili kwa madai kwamba haina soko nzuri kutokana na kwamba inapatikana kwa urahisi maeneo haya,” anaeleza Bahati wakati wa mahojiano.

Kulingana naye, aliamua kuzamia kilimo hiki baada ya kufanya utafiti wa kina na kugundua kwamba aina hii ya pilipili haipatikani maeneo yote Pwani kama baadhi wanavyodhania.

Bahati aliamua kutenga sehemu ndogo ya shamba lake kupanda aina hii ya pilipili kujaribu na baada ya miezi miwili alianza kuona matokeo.

“Baada ya miezi miwili pekee , pilipili zangu zilikuwa zikinawiri shambani ila tatizo ni kwamba sikuweza kupata soko la haraka kuuza mazao yangu.”

Lakini matokeo mazuri ya mazao yalimpatia motisha kusaka wateja hasa katika mahoteli ya kitalii yaliyo karibu na eneo la Kanamai na Kilifi hata kufaulu kupata kwa wafanyibiashara wa reja reja na wa jumla.

Mapema mwaka 2020, Bahati aliamua kuongeza robo ekari ya shamba lake kuendeleza ukuzaji wa pilipili.

Anasema kuwa aina hii ya pilipili hufanya vyema sana kipindi cha mvua kuliko kiangazi ambapo huvamiwa na magonjwa na kutatiza ukuaji wake.

Na tofauti na pilipili za kawaida zinazochukua kipindi cha kati ya miezi minne hadi mitano, aina hii ya pilipili hucuhukua miezi miwili pekee kukomaa.

Katika shamba lake la robo ekari, Bahati anasema kwamba yeye huvuna hadi kilo 20 kwa siku huku akiuza kilo moja kwa kati ya Sh70 hadi 80 kulingana na hali ya soko.

Bahati mwenye umri wa miaka 46, asema pilipili hii ya kienyeji ina faida tele kwa kuwa mkulima anaweza kuvuna kwa kipindi cha mwaka mmoja kabla ya kuamua kuing’oa na kupanda mingine.

Kati ya changamoto anazokabiliana nazo zinaibuka kipindi cha mavuno ambapo humchukua kipindi kirefu kuvuna kutokana na udogo wa pilipili.

You can share this post!

AKILIMALI: Maparachichi aina ya hass yamvunia kipato katika...

Fatma ataka klabu za akina dada zijiunge kushiriki ligi ya...