• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 5:55 AM
Fatma ataka klabu za akina dada zijiunge kushiriki ligi ya Kwale

Fatma ataka klabu za akina dada zijiunge kushiriki ligi ya Kwale

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

KLABU zinazotaka kushiriki kwenye Ligi ya FKF Kaunti ya Kwale zimepewa hadi Oktoba 15, 2021, kuthibitisha kushiriki ili zipangwe kwenye ratiba ya ligi hiyo inayotarajia kuanza rasmi hapo Oktoba 23, 2021.

Mwakilishi wa soka ya akina dada wa Shirikisho la Soka la Kaunti ya Kwale, Fatma Tuli amesema ni klabu tano pekee hadi sasa ndizo zimethibitisha kushiriki kwenye ligi ya kaunti hiyo na akatoa ombi kwa klabu nyingine zijitokeze na kuthibitisha kushiriki kwao.

Akizungumza na Taifa Leo kwa njia ya simu, Fatma amesema kuwa klabu tatu ambazo tayari zimeshathibitisha kushiriki katika ligi hiyo kutoka kaunti ndogo ya Msambweni ni Ukunda Queens, Barcelona na Ukunda Starlets.

Amesema klabu mbili za kaunti ndogo ya Lungalunga ambazo zimeshakubali kushiriki ni Lungalunga United Ladies FC na Dogo Dogo Ladies FC.

“Ninaamini klabu nyingi zaidi hasa kutoka kaunti nyingine ndogo za Kinango na Matuga zitajitokeza kushiriki,” akasema Fatma.

Fatma alisema mwisho wa kuthibitisha kushiriki kwenye ligi hiyo ni Oktoba 15 na siku itakayofuatia asubuhi kutafanyika mkutano hapo Kombani baina ya maafisa wa FKF Kwale na wawakilishi wa klabu za Msambweni na Matuga.

Siku hiyo hiyo ya Oktoba 16 saa nane mchana kutakuwa na mkutano wa klabu za Lungalunga na maafisa wa FKF Kwale utakaofanyika Kibaoni.

Mnamo Oktoba 17, 2021, kutakuwa na mkutano kama huo lakini na klabu za Kinango ambao utafanyika mjini Samburu.

You can share this post!

AKILIMALI: Pilipili kali inayoogopwa na wenyeji kwa mwasho...

TAHARIRI: Serikali iwakinge wananchi maskini